Friday, 26 January 2018

MSIGWA AWAKUMBUKA JAH PEOPLE NA JESCA, CHADEMA IKIILALAMIKIA CCM NA POLISIMBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amemkumbuka Jah People, Dk Jesca Msambatavangu na Abeid Kiponza akisema wakati wa uongozi wao ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), vyama vya upinzani hawakuvifanya maadui kama ilivyo sasa.

“Tumefanya siasa na Jah People, Kiponza na Jesca, ilikuwa ni kawaida tukimaliza siasa tunapena mikono, na mambo mengine yanaendelea pasipo hila yoyote,” Mchungaji Msigwa aliyasema hayo  kwa wanahabari leo alipokuwa akizungumzia mustakabali wa kisiasa mjini Iringa na kamatakamata aliyosemwa inafanywa na jeshi la Polisi kwa wana Chadema kwa lengo la kukibeba Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema ametoa malalamiko kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro na Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI), Robert Boaz yanayohusisha Jeshi la Polisi Mkoani hapa kufanya kazi kwa maelekezo ya CCM.

Alisema hivikaribuni jeshi hilo liliwakamata wafuasi wa chama chake kwa maelekezo ya CCM na kuwafikisha mahakamani baada ya siku nane, wakiwahusisha na tukio la kuvunja nyumba ya diwani wa kata ya Mwangata aliyejiuzulu, Anjelus Mbogo na kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM Iringa Mjini, Alphonce Muyinga; bila kufanya uchunguzi.

Katika kesi hizo, Mchungaji Msigwa alisema amehusishwa pia katika kesi ya kuchoma nyumba ya katibu huyo katika tukio lililotokea yeye akiwa nje ya mkoa wa Iringa.

“Waliponiita Polisi niliwaambia sikatai waharifu wanaweza kuwepo Chadema, lakini pia wanaweza kuwepo CCM, wasio na vyama, na matukio kama hayo yanaweza kuwa ya kupangwa na wahusika kwa malengo ya kisiasa au ya kiuchumi kwahiyo kabla ya kamata kamata ni muhimu  Polisi wakafanya kazi yao kwa weledi na utulivu,” alisema.

Mchungaji Msigwa alikwenda mbali akisema anazo taarifa (hakusema kazipata wapi) kwamba matukio hayo yanatengenezwa na CCM kwa lengo la kuichafua Chadema baada ya mipango yao ya kuwashawishi na kuwanunua baadhi ya madiwani wa chama hicho kuanza kuonekana hayawaongezei umaarufu.

Pamoja na chama hicho kuitaka halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa udi na uvumba, alisema pia kinataka jimbo la Iringa Mjini kwa nguvu zake zote na kwamba ipo mipango mingine (hakusema inafanywa na nani) ya kuhakisha anatengenezewa kesi itakayomfunga.

 “Iringa siwezi kuondoka kwa mkono wa mtu nitaondoka kwa mapenzi ya Mungu, mwanadamu hawezi kuniondoa, niliweka kwa mpango wa Mungu na nitaondoka kwa mpango wa Mungu,” alisema.

Msigwa alisema kasi ya wakazi wa manispaa ya Iringa kuikataa CCM ilipamba moto wakati wa Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 ilipopoteza mitaa 65 na ikaendelea kwa nguvu kubwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ilipopoteza halmashauri na jimbo la Iringa kwa mara ya pili mfululizo.

Mchungaji Msigwa aliwaomba radhi wananchi akisema madiwani waliojiuzulu na kukimbilia CCM wamefanya hivyo kwasababu ya njaa zao ambazo hazikuonekana wakati wakiteuliwa kugombea udiwani katika uchaguzi huo.

Alisema Chadema itasimamisha wagombea madhubuti katika kata nne za Ruaha, Mwangata, Mkwawa na Kwakilosa ambazo madiwani wake walijiengua na kujiunga na CCM kwa nyakati tofauti hivikaribuni kauli inayotengua msimamo wao wa awali wa kususia chaguzi ndogo.

Katika chaguzi za kata hizo, Mchungaji Msigwa alisema hawatakubali haki yao kudhulumiwa kama ilivyokuwa katika uchaguzi mdogo wa kata ya Kitwiru aliodai kwamba yalitengenezwa mazingira nje ya utaratibu kuiwezesha CCM kushinda.

Pamoja na kupoteza kata ya Kitwiru, Chadema pia ilipoteza kata ya Kihesa baada ya kususia uchaguzi huo uliompa ushindi wa bila kupinga mgombea wa CCM July Sawani.


Jitihada za mtandao huu kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Julius Mjengi kuzungumzia tuhuma hizo hazikuzaa matunda, lakini zitaendelea tena kesho ili kupata upande wa pili wa madai haya .

Reactions:

0 comments:

Post a Comment