Tuesday, 23 January 2018

MNEC ASAS AWAELEZA VIJANA WA IRINGA WAPI FURSA ZAO ZIPO

Image result for salim asas


MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Salim Abri Asas amewataka baadhi ya wakazi wa manispaa ya Iringa hususani vijana wanaochukia watu wanaochangia maendeleo kubadili mitazamo hiyo ili wawe sehemu ya maendeleo ya mji wao.

“Mwenyekiti kuna mtu aliniambia, na sijui kama ni kweli kwamba wewe kama ni kiongozi hapa manispaa na ukitaka kupendwa basi tukanatukana…..na usilete maendeleo,” alisema akimwambia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) Taifa, Kheri James aliyepo kikazi mkoani Iringa kujionea uhai wa umoja huo.

Katika mkutano ulioandaliwa na UV-CCM Mkoa wa Iringa katika Jumba la Maendeleo Mjini Iringa na kuhudhuriwa na viongozi, wanachama na wapenzi wa umoja huo kutoka wilaya zote za mkoa wa Iringa mapema leo, Asas alisema ukitaka kuchukiwa katika manispaa hiyo basi shiriki kuleta maendeleo na jitokeze kusaidia saidia watu.

Aliwaomba watu wenye tabia hiyo wabadilike na washirikiane na wadau wengine kuzitumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.

“Nataka niwaambie fursa kwa vijana zipo ndani ya CCM, nje ya CCM mtadanganyana tu, mtapaje fursa?....kwanini nasema fursa zipo ndani ya CCM ni kwasababu ndicho chama kinachotawala…..CCM ni serikali,” alisema huku akiuliza kama kuna kijana amepata fursa nje ya CCM ajitokeze.

“Ujumbe huu nauelekeza kwa vijana waliopo ndani ya manispaa hii ya Iringa, waje wanieleze, wanikalishe……kwamba bwana eeh sisi tumepata fursa nje ya CCM, waje wanieleze hapa, waje watukalishe sisi wana CCM wote watwambiwe hizo fursa walizopata nje ya CCM ni zipi na kama hakuna kwanini wanafanya ushabiki,” alisema huku akiwataka vijana hao wabadilike.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment