Friday, 26 January 2018

MLOWE, SAWANI WATAJWA KUMSHAWISHI MEYA IRINGA AACHIE NGAZI

Image result for Meya wa Manispaa ya IringaAlex Kimbe

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe (Chadema) amewataja makada wa wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Michael Mlowe na July Sawani akisema wamekuwa wakimshawishi kwa ahadi ya kumpa fedha ili aachie wadhifa huo, tuhuma ambazo wawili hao wamezikanusha huku wakiahidi kukutana na wanahabari hivikaribuni na kutoa ufafanuzi.

Wakati Mlowe ni mmoja kati ya makada wa CCM waliojitokeza katika kura za maoni za chama hicho kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Sawani ni Diwani mteule wa kata ya Kihesa anayesubiri kula kiapo baada ya kupita bila kupingwa katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kihesa uliofanyika Januari 13.

Image result for Diwani July Sawani

Akizungumza na wanahabari leo akiwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mwenyekiti wa Bavicha, Leonce Marto; Kimbe alisema watu hao wanapoteza muda wao bure na akawaomba wasimpigie simu tena kwa jambo hilo.

Meya huyo aliye hatarini kupoteza kiti hicho kwasababu ya kukimbiwa na madiwani wengi wa chama chake alisema Januari 12, mwaka huu alipigiwa simu na  Mlowe na Sawani na akakutana nao Miami Bar akijua wana mazungumzo ya kawaida badala yake walifanya ushawishi huo ili aachie kiti chake hicho.

“Pamoja na fedha nyingi walizoniahidi niliwaambia haziwezi kuwa na thamani ya kura na heshima waliyonipa watu wa Iringa,” alisema.

Katika maelezo yao Kimbe alisema wawili hao walimwambia CCM inahitaji  madiwani wawili tu kwasasa ili iweze kuchukua halmashauri hiyo.

Hiyo ni baada ya madiwani sita kati ya 14 waliochaguliwa kupitia Chadema kujitoa katika chama hicho na kujiunga na CCM ambayo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ilishinda kata nne tu kati ya 18.

Pamoja na wawili hao, Kimbe alisema amekuwa akipigiwa simu na watu wengine asiowajua wakimuahidi kumpa Sh Milioni 200 ili aachie ngazi, kiasi cha fedha alichosema amekikataa kwasababu ya heshima aliyopewa na wana Iringa.


Pamoja na uchache wao katika baraza la madiwani hivi sasa, aliwaomba wananchi wa manispaa hiyo kuendelea kuwaamini akisema wataendelea kuwahudumia kama walivyopanga.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment