Monday, 29 January 2018

MEYA IRINGA KUWEKA WAKILI KESI YA KUTISHIA KUUA ITAKAPOANZA FEBRUARI 5


MEYA wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe (Chadema) atapanda katika kizimba cha mahakama ya wilaya ya Iringa Februari 5 mwaka huu kuanza kujibu tuhuma za kutishia kumuua kwa bastola Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV-CCM), Alphonce Muyinga.

Kesi hiyo inaanza kusikilizwa baada ya Wakili wa Serikali Alex Mwita mapema leo kuileza mahakama hiyo kwamba upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 189 ya mwaka 2017 Kimbe anashitakiwa kutishia kumuua kiongozi huyo wa UVCCM kinyume na kifungu namba 89 (2) (a) cha kanuni za adhabu.

Meya huyo anatuhumiwa kutenda kosa hilo katika maeneo ya kata ya Kitwiru mjini Iringa wakati wananchi wa kata hiyo wakipiga kura ya kumchagua diwani wao katika uchaguzi mdogo wa kata hiyo uliofanyika Novemba 26, mwaka jana.

Akizungumza na wanahabari baadaye Kimbe ambaye awali alipanga kujitetea mwenyewe katika kesi hiyo alisema anawasiliana na chama chake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili apate wakili.

“Haya ni mambo ya kisheria nadhani nina haja ya kuwa na wakili katika shauri hili,” alisema mbele ya wafuasi kadhaa wa chama hicho waliojitokeza kumsindikiza mahakamani hapo jana.

Kwa mara ya kwanza kesi hiyo inayovuta hisia za wafuasi wa vyama vya siasa mjini Iringa ilifikishwa katika Mahakama hiyo Novemba 28, mwaka jana na toka wakati huo ilitajwa mara nne kwa kuwa upelelezi wake ulikuwa haujakamilika.


Wakati Kimbe akihudhuria mara zote wakati shauri hilo likitajwa, mlalamikaji katika kesi hiyo Alphonce Muyinga hajawahi kuonekana mahakamani hapo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment