Thursday, 11 January 2018

KESI YA MEYA MANISPAA YA IRINGA YAPIGWA TENA KALENDAMSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe anayetuhumiwa kutishia kuua kwa kutumia bastola atapanda katika kizimba cha Mahakama ya Wilaya Iringa Januari 29, 2018 baada ya mapema leo hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama hiyo, Richard Kasele, kuihairisha tena ikiwa tayari imekwishatajwa mara tatu.

Kesi hiyo ya jinai namba 189 ya mwaka 2017 iliyoelezwa na Wakili wa Serikali, Alice Thomas kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, ilifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Novemba 28, mwaka jana.

Kimbe anashitakiwa kutenda kosa hilo Novemba 26 mwaka jana katika kata ya Kitwiru mjini Iringa wakati wananchi wa kata hiyo wakipiga kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo.

Katika kesi hiyo Kimbe anashitakiwa kutishia kumuua kwa bastola Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV CCM) Manispaa ya Iringa, Alphonce Muyinga kinyume na kifungu namba 89 (2) (a) cha kanuni za adhabu.
  
Wakati Meya huyo akisubiri kujitetea katika kesi hiyo, chama chake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Iringa kinaendelea kupata nyufa zinazozidi kukisambaratisha.

Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, idadi ya madiwani waliochaguliwa atika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kupitia chama hicho imepungua kutoka 14 hadi tisa, hiyo ikiwa ni baada ya madiwani watano wa kata ya Kitwiru, Kihesa, Ruaha, Kwakilosa na Mwangata kwa nyakati tofauti kutangaza kujitoa katika chama hicho na kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM).


Pamoja na madiwani hao wa kuchaguliwa, chama hicho kimepoteza pia madiwani wa viti maalumu watatu kati ya watano kilionao ambao hata hivyo nafasi zao zitajazwa kwa kuzingatia orodha ya madiwani wa viti maalumu waliopelekwa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment