Thursday, 25 January 2018

KAYA MASIKINI IRINGA VIJIJINI ZATUMIA FURSA YA TASAF KUPAMBANA NA HALI ZAOKAYA 37 zinazonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika kijiji cha Makombe wilayani Iringa zimewekeza katika kilimo cha mahindi na korosho, zikilenga kwa pamoja kutumia fursa hiyo kujikwamua na umasikini katika kipindi kifupi kijacho.

Pamoja na kilimo hicho, Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Fredy Mnyawami alisema kaya hizo zinafuga kuku wa kienyeji, sungura na bata.

“Wanalima ekari 49 za mahindi, na wana ekari tano za mikorosho lakini pia wana kuku 201 wa kienyeji, sungura 13 na bata 12,” alisema Mnyawami.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alizitembelea kaya hizo juzi na kuzipongeza kwa kuzingatia masharti ya fedha wanazopata kupitia mpango huo.

Alisema mpango huo ni muhimu kwa vile unawezesha kaya za walengwa kupata kipato zaidi, unatengeneza fursa zingine  na unawapatia walengwa weledi na stadi za mbalimbali wakati wa utekelezaji miradi.

“Utekelezaji wa mpango huu haulengi tu katika kuhawilisha fedha kwa walengwa bali pia unahimiza ushiriki wa walengwa katika kazi za mikono kupitia miradi ya mbalimbali katika maeneo yao ili waweze kupata kipato, na kuwekeza” alisema.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Donald Mshani alisema halmashauri iliingia katika awamu ya tatu ya mpango huo (TASAF awamu ya tatu) Januari 2015 na hadi Januari, mwaka huu imekwishapokea zaidi ya Sh Bilioni 5.1 kwa ajili ya kuziwezesha kaya lengwa, usimamizi na ufuatiliaji.

Alisema sehemu ya fedha hizo zimetumiwa na kaya hizo kuanzisha miradi midogo ya ufugaji, kilimo, ujenzi na vikundi vya kuweka na kukopa, maarufu kama Vicoba.

“Jumla ya kaya 8,137 kutoka vijiji 82 kati ya 133 vya halmashauri hii zipo kwenye utekelezaji wa mpango,” alisema.

Akiwa katika kijiji hicho cha Makombe, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alipata fursa ya kumtembelea Mary Msigwa ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mpango huo.

Msigwa alimuonesha mkuu wa mkoa nyumba ndogo ya tope iliyoezekwa kwa nyasi aliyokuwa akiishi kabla ya kuingia katika mpango huo na nyumba yake mpya ambayo amejenga kwa tofali mbichi na kuezeka kwa bati kutokana na akiba ya fedha anazopata kupitia mpango huo.

Mkuu wa mkoa na ujumbe aliombatana nao walichanga zaidi ya Sh 126,000 zitakazomuwezesha mlengwa huyo kununua sementi atakayotumia kusakafia nyumba hiyo ya vyumba viwili vya kulala na kuboresha muonekano wake.


Kwa kupitia mpango huo, baadhi ya walengwa wameweza pia kujiunga na mfuko wa bima wa afya ya jamii (CHF), na watoto wao kunufaika na mpango wa elimu na afya kwa kutimiza masharti.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment