Thursday, 18 January 2018

IRINGA VIJIJINI WAANZA KULIMA KOROSHO


HALMASHAURI ya wilaya ya Iringa imeanzisha kilimo cha korosho kama zao mbadala la biashara la halmashauri hiyo inayolima pia tumbaku na mpunga kwa wingi.

Kilimo cha zao hilo kilizunduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza jana katika kijiji cha Idodi, wilayani humo.

Mbali na kijiji cha Idodi, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Robert Masunya alitaja vijiji vingine ambavyo zao hilo linaweza kustawi vizuri kuwa ni Mahuninga, Mlowa, Ilolompya, Mlenge, Itunundu, Kising’a, Kihorogota, Nyang’oro, Nzihi na Kiwele.

Masunya alisema kwa udhamini wa Bodi ya Korosho, halmashauri hiyo imezalisha miche 69,855 itakayotolewa bure kwa taasisi za elimu (shule za msingi na sekondari) na kwa wananchi wenye mashamba yaliyo tayari kwa ajili ya kupandwa msimu huu wa kilimo.

Kwa kupitia awamu ya kwanza ya mpango huo wa uanzishaji wa kilimo cha zao hilo, mkurugenzi huyo alisema shule za msingi zitapewa miche 3,672 itakayopandwa katika mashamba yao yenye ukubwa wa ekari 136.

“Na shule za sekondari zitapewa miche 378 kwa ajili ya ekari 14 na wananchi watapewa miche 65,803 itakayooteshwa katika ekari 2,437,” alisema. 

Afisa kilimo wa halmashauri hiyo, Lucy Nyalu alisema mbegu zinazotolewa kwa wananchi na taasisi hizo ni za muda mfupi zitakaoanza kutoa mazao baada ya miaka mitatu.

Wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo akisema; “Kuanzishwa kwa zao hili wilayani Iringa ni fursa kubwa itakayousaidia mkoa na watu wake kupambana na umasikini na kuongeza mapato yake.”

Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alizungumzia bei ya zao hilo akisema taarifa za hivikaribuni zinaonesha kilo moja ya korosho zilizobanguliwa inauzwa hadi Sh 4,000.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka maafisa ugani na viongozi wa vijiji, kata na tarafa zinazolima zao hilo kutimiza wajibu wao ili kukifanya kilimo cha zao hicho kiwe chenye tija.

“Tunataka mkoa ufanikiwe katika kilimo cha zao hili na ushauri wangu itungwe sheria ndogo itakayomlazimisha kila mkulima kushiriki katika kilimo hiki kinachotarajiwa pia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kubangua korosho,” alisema.


“Lakini pia nataka kuona viongozi wa vijiji katika maeneo husika wanakuwa wa mfano kwa kuwa na mashamba darasa ambayo wananchi wengine watayatumia kujifunza,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment