Thursday, 4 January 2018

IDARA YA ELIMU YA JUMUIYA YA WAZAZI WA CCM YAJITOSA VITA DHIDI YA UKATILIJUMUIYA ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kupitia idara yake ya Elimu, Malezi na Mazingira imeanza kampeni ya kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji vinavyofanywa kwa watoto wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, mjini Iringa.

Akizungumza na mtandao huu jana, katibu wa idara hiyo,  Bovan Mwakiyambiki alisema kumekuwepo na taarifa za ongezeko la wanafunzi wa shule hizo wanaobakwa na kulawitia kwasababu mbalimbali zikiwemo imani za kishirikina.

“Tumetembelea baadhi ya shule za msingi za manispaa ya Iringa, simulizi tulizokutana nazo zinasikitisha na kwa kweli zinaongeza haja ya kampeni hiyo na ushiriki wa vyombo vya dola ili kumaliza tatizo hilo,” alisema.

Alisema uchunguzi wa idara yao unaonesha yapo baadhi ya matukio ya ubakaji na ulawiti yanayoropitiwa Polisi lakini pia yapo mengine mengi ambayo hayafikishwi katika chombo hicho cha dola.

“Baadhi ya watoto na wakati mwingine kwa kushirikiana na wazazi wao, wanaficha taarifa za matukio haya kitendo kinachofanya baadhi ya watoto wazoee kufanyiwa vitendo hivyo na kuwa walimu wa watoto wenzao,” alisema.

Pamoja na jumuiya hiyo kutangaza kulivalia njuga tatizo la ubakaji na ulawiti, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza na viongozi wengine wa serikali wameendelea kutoa maagizo mbalimbali kufanikisha mikakati ya kutokomeza tatizo hilo.

Akizungumza na viongozi wa dini hivikaribuni,  Masenza aliwaomba kuwahamasisha waumini wao kuwajali watoto wao na wakati mwingine kutowalaza chumba kimoja na wageni, kwani baadhi ya taarifa zinazoripotiwa zinaonesha vitendo hivyo hufanywa na baadhi ya ndugu katika familia. 

Masenza aliwaomba Wanajamii pia kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao kila jioni ili kujua changamoto zinazowakabili, na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kuzuia madhara makubwa yanayowakumbumba watoto, ikiwemo kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa vitendo hivyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alitoa waraka wa kuzuia watoto kutembea au kutumwa mahali popote pale wakati wa usiku na kutembea umbali mrefu bila wasaidizi wao.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Iringa, David Ngunyale alisema kumekuwa na ongezeko la kesi za unyanyasi wa kijinsia hususani za vitendo vya ubakaji na ulawiti zinazofunguliwa mahakamani hapo.

Alisema wakati mwaka 2016 kulikuwa na jumla ya kesi 62 za ubakaji na ulawiti, Januari hadi Juni mwaka 2017 kulikuwa na kesi 36.

Kwa niaba ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), Deusdedit Kasindo alisema matukio ya ubakaji na ulawiti mkoani Iringa yamekuwa yakisababishwa na ulevi ukiwemo wa kutumia dawa za kulevya, tama ya mapenzi, ushirikina, kutekelezwa kwa watoto na umasikini.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment