Monday, 8 January 2018

DC AFIKISHA SALAMU ZA MAENDELEO KWA WANA KILOLO WAISHIO DAR
MKUU wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah amekutana na wana Kilolo zaidi ya 200 waishio jijini Dar es Salaam katika mkutano alioutumia kunadi fursa za wilaya hiyo zinazoweza kuchochea uchumi wa viwanda na ukuaji wa sekta zingine.

Katika mkutano huo uliofanyika jana kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine Magomeni, Abdallah aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto, mkurugenzi wa Halmashauri na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo.

“Mtu wa kwanza kuijenga wilaya ya Kilolo ni mwana Kilolo mwenyewe, tumeamua kuwafuata Dar es Salaam ili tufahamiane na kuwakumbusha umuhimu wenu na ushiriki wenu katika kuzitumia fursa hizo kuleta maendeleo,” alisema.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya shughuli hiyo ya uhamasishaji kufanyika kwa kiwango cha kuridhisha ndani ya mipaka ya wilaya hiyo na kuanza kuonesha mafanikio.

Alisema katika sekta ya kilimo, wilaya ya Kilolo ina ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara ambayo kwa wingi wake yanaweza kuchochea uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.

“Kilolo tunalima nyanya, vitunguu, viazi, mahindi na matunda ya aina mbalimbali kwa wingi, tuna miundombinu ya umwagiliaji, mito mingi na hali ya hewa nzuri inayofaa pia kwa kilimo cha chai, pareto na miti, na ufugaji ukiwemo wa nyuki na samaki,” alisema.

Aidha alizungumzia mabadiliko makubwa katika sekta nyingine ikiwemo ya afya, elimu, maji, utalii, mundombinu, nishati na umeme, na mawasiliano akisema kwa pamoja ni muhimu katika kufikia malengo ya wilaya hiyo.

Akizungumzia mazingira ya uwekezaji, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Aloyce Kwezi alisema wana ardhi kubwa ikiwemo ile inayofaa kwa kilimo cha uwagiliaji na kuna maeneo na viwanja vya kutosha kwa ajili ya uwekezaji wa miradi mbalimbali na nyumba za makazi.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo hilo, Venance Mwamotto alisema; “Tunaridhishwa na kasi iliyopo ndio maana tunawafuata wadau wetu wengine nje ya wilaya. Kama mbunge wajibu wangu ni kuisukuma serikali kuzishughulikia kero mbalimbali zinazokwamia au kuchelewesha maendeleo. Niipongeze serikali kwani katika eneo hili inajitahidi sana.”

Wakiitikia wito wa kurudi na kuindeleza wilaya hiyo, wananchi hao walichanga zaidi ya Sh Milioni 8, fedha taslimu na ahadi, ili kusaidia kuboresha sekta ya elimu na afya, waliyosema ni muhimu kwa ukuaji wa mandeleo ya wilaya na wakakubalina kukutana mara mbili kwa mwaka ili kufanya marejeo ya ushiriki wao.

Aidha, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Profesa Joe Lugalla ambaye ni mmoja a wadau wa maendeleo ya wilaya hiyo aliahidi kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo kwa kuandika maandiko ya miradi mbalimbali inayohitaji msaada wa fedha kutoka kwa wahisani kama njia ya kuharakisha utafutaji na upatikanaji wa fedha hizo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment