Friday, 5 January 2018

CHADEMA IRINGA YAPATA MSIBA MWINGINE, DIWANI, KATIBU WAIKIMBIA


DIWANI wa kata ya Mwangata Jimbo la Iringa Mjini, Anjelusi Mbogo na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Iringa, Oscar Ndale wametangaza kujiuzulu nafasi zao sambamba na kujivua uanachama wa chama hicho leo.

Mbogo anakuwa diwani wa saba wa chama hicho mjini hapa (madiwani watano wakuchaguliwa na wawili wa viti maalumu) kufanya maamuzi hayo ndani ya miezi minne.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Chadema ilizoa viti 14 kati ya 18 vya udiwani  na ikabeba jimbo la Iringa Mjini kwa mara ya pili mfululizo kupitia mgombea wake, Mchungaji Peter Msigwa.

Akieleza sababu za kujitoa katika chama hicho jana, Mbogo alisema ameshindwa kuvumilia vurugu za kiuongozi zinazofanywa na Mchungaji Msigwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa.

Alisema viongozi hao wanaongoza chama hicho kama miungu watu, wababe na hawaambiliki jambo linalowazidishia jeuri ya madaraka na maamuzi ndani ya  chama na katika vikao vya madiwani wa chama hicho.

 “Hakuna afya tena ndani ya Chadema, kufanya kazi chini ya watu hawa wawili ni tatizo na kujinyima raha. Natangaza kujitoa Chadema lakini kama viongozi hao wataachia ngazi nyadhifa zao, nipo tayari kurudi na kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema.

Naye Ndale alisema amejitahidi kwa uwezo wake wote kushughulikia migogoro ya Iringa Mjini lakini makao makuu wamekuwa wakiifumbia macho na kufanya kila baada ya muda fulani litokee jambo jingine lisilo na afya kwa chama jambo linalozidi kuwapotezea muda ndani ya chama hicho.

Alisema Mchungaji Msigwa amekuwa ni kiongozi jeuri na mwenye roho mbaya ambaye kila anapopingwa au kukosolewa amekuwa akiwaaita wanaofanya hivyo wasaliti na wenye njaa.

“Yawezekana kweli tuna njaa, lakini nadhani njaa yake ni kubwa zaidi kwani pamoja na kupata marupurupu mengi kwa kupitia nafasi yake ya ubunge mchango wake wa kifedha kwa shughuli na maendeleo ya chama ni mdogo wakati mwingine kuliko wanachama wa kawaida,” alisema.

Ndale alisema Mchungaji Msigwa ameteka majukumu ya chama katika jimbo hilo na mkoa wa Iringa kwa ujumla na mambo mengi yamekuwa hayawezi kufanyika bila maelekezo yake, jambo ambalo limedhohofisha mapenzi na hali ya viongozi na wanachama wengine kufanya kazi za chama hicho.

“Hata pale viongozi wa kitaifa wanapokuja akiwemo Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk Vicent Mashinji, badala ya kuwasiliana na viongozi wa chama mkoa wamekuwa wakiwasiliana na mbunge huyo,” alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka minne tangu awe katibu wa Chadema wa mkoa huo hajawahi kupata fursa ya kuzungumza na viongozi wa kitaifa kila wanapokuja mkoani Iringa kwani wamekuwa wakikumbatiwa na mbunge huyo na hivyo kukosa au kutoona haja ya kukutana na viongozi wengine wa mkoa.

“Viongozi wa kitaifa wanapokuja mkoani Iringa mwenyeji wao ni mwenyekiti na katibu wa mkoa, lakini Chadema, jukumu hilo limekuwa la Mchungaji Msigwa,” alisema.

Alisema katika mazingira ambayo viongozi wa ngazi zote mkoani wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kujitolea, ni jambo linalosononesha pale mamlaka zao zinapopuuzwa.

Akizungumzia mgawanyo wa ruzuku ya chama mikoani, Ndale alisema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, amewahi kupokea Sh 100,000 tu toka makao makuu.

“Sasa najiuliza swali, kazi hii kubwa tunafanya kwa kujitolea na kwa kutumia rasilimali zetu, za wanachama na wafuasi wengine halafu hata yale tunayoshauri au kukubalina kwenye vikao halali kwanini yanashindwa kufanyiwa kazi na uongozi wa kitaifa,” alihoji.

Alisema kama viongozi wa kitaifa hawatasikia kilio cha wanachama na wapenzi wa Chadema wa mjini Iringa dhidi ya tabia, hulka na mambo yanayofanywa na Mchungaji Msigwa kwa maslai yake binafsi, hakuna ubishi kwamba chama hicho kitapotea katika ramani muda si mrefu.

Alisema kwasababu hizo na nyingine nyingi ambazo hawezi kuzimwaga hadharani kwasasa ameamua kujitoa katika chama hicho na amekwishatuma maombi ya kujiunga na CCM.


Pamoja na viongozi hao, Katibu wa Chadema wa Kata ya Mwangata, Tumaini Gwivaha naye ametangaza kujivua unachama wa chama hicho na kukimbilia CCM akisema amechoka kutumika kama punda kwa maslai ya watu wachache.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment