Wednesday, 3 January 2018

CHADEMA IRINGA MJINI YAENDELEA KUBOMOKA, MADIWANI WENGINE WAWILI WATIMKA


NGOME ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Iringa Mjini imebomoka tena leoa baada ya madiwani wake wawili, Joseph Lyata wa kata ya Kwakilosa na Tendesy Sanga wa kata ya Ruaha kutangaza kwa nyakati tofauti kujivua wadhifa huo sambamba na kujiengua uanachama wa chama hicho.

Wakati Lyata alizungumza na wanahabari mjini Iringa leo, Sanga alisambaza taarifa yake ya kujiuzulu katika vyombo mbalimbali vya habari mjini Iringa na jijini Dar es Salaam.

Sanga na Lyata aliyetangaza kusudio lake la kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wowote kuanzia sasa, wanafanya jumla ya madiwani wa Chadema Iringa Mjini kujiengua na chama hicho kuwa sita.

Wengine waliojiengua na kujiunga na CCM mwaka jana ni Baraka Kimata aliyekuwa diwani wa kata ya Kitwiru, Edger Mgimwa wa kata ya Kihesa na madiwani wawili wa viti maalumu Leah Mleleu na Husna Daudi.

Akitangaza uamuzi huo leo, Lyata alimtuhumu Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Nyasa (Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini) akisema anaua demokrasia ndani ya chama hicho na maamuzi yake ni ya kibabe yasiyozingatia katiba na maamuzi ya pamoja.

“Mbowe kama ataicha Iringa hivi hivi asitegemee kuiona Chadema tena. Kuna madiwani wengine wengi watajitoa kwasababu Mchungaji Msigwa anapokosolewa, anawatangaza wanaomkosoa kwamba ni wasaliti na baadaye anawatenga kwenye shughuli mbalimbali za chama na maendeleo ya kata na jimbo,” alisema.

Alizitaja sababu mbili zilizomfanya ashindwe kuvumilia kuendelea kuwa mwana Chadema na diwani kwa kupitia chama hicho kuwa ni pamoja na migongano na kutofuatwa kwa mifumo rasmi ya uendeshaji wa baraza la madiwani na ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chadema.

Lyata aliyekuwa naibu meya wa manispaa ya Iringa mwaka 2017 alizungumzia namna Mchungaji Msigwa alivyouvuruga maamuzi ya madiwani wa chama hicho waliomtaka aendelee kuwa naibu meya kwa miaka mitano na jinsi alivyoharibu mchakato wa kupata viongozi wa kanda ya Nyasa kwa nyakati tofauti mwaka jana.

“Wapo watakaosema nimenunuliwa na CCM kwasababu hii ndio lugha ya Chadema wanaojinasibu kunadi demokrasia. Lakini ukweli ni kwamba mimi sijanunuliwa na mtu yoyote wala chama chochote. Mimi nina kazi zangu, kitaaluma ni mwalimu, mke wangu ana kazi yake na tuna shughuli zingine za kiuchumi tunazofanya zinazotuingizia kipato,” alisema.

Wakati uamuzi wa diwani huyo ukielezwa kuwakasilisha wafuasi wa Chadema; CCM imeupokea kwa furaha iliyoelezwa na mwenyekiti wake wa Iringa Mjini Said Rubeya kwamba unawapunguzia machungu ya kupoteza Jimbo la Iringa Mjini na halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, CCM ilipoteza kwa mara ya kwanza katika historia yake halmashauri ya manispaa ya Iringa baada ya kupata madiwani wanne kati ya 18 wa jimbo hilo na ikapoteza kwa mara ya pili Jimbo la Iringa Mjini kwa Mchungaji Msigwa.

Katika barua yake ya kujiuzulu (nakala tunayo), Sanga amesema amefikia uamuzi huo kwakuwa haridhishwi na mwenendo wa Chadema na jinsi baraza la madiwani la halmshauri hiyo linavyoendeshwa.

Hadi tunakwenda mitamboni, Mchungaji Msigwa hakuweza kupatikana kuzungumzia uamuzi wa madiwani hao na tuhuma dhidi yake, na taarifa kutoka kwa watu walio jirani naye walisema yupo kwenye kikao kizito cha chama.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment