Monday, 15 January 2018

ASAS ATOA AHADI TATU ZA MAENDELEO SAWANI AKIPEWA HATI YA UDIWANI


MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anayewakilisha mkoa wa Iringa, Salim Asas amefanya mkutano wa kwanza wa hadhara mjini Iringa jana na kutoa ahadi za maendeleo tatu, zinazokuwa za kwanza kutamkwa hadharani tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwezi mmoja uliopita.

Ahadi hizo ambazo utekelezaji wake unaanza wiki hii ni pamoja na kumalizia ujenzi wa jengo la kitega uchumi la kata ya Kihesa linalojengwa pembeni mwa ofisi ya kata hiyo na kuchangia mifuko 200 ya sementi kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya ya shule ya sekondari ya Kihesa.

Ahadi ya tatu ambayo pamoja na nyingine za kwanza ilipokewa kwa nderemo la vifijo kutoka kwa mamia ya wapenzi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliofurika katika mkutano huo uliofanyika mbele ya ofisi ya kata hiyo ni ya kuchangia shughuli za ujasiriamali zinazotengeneza ajira kwa vijana wa kata hiyo.

Asas alitoa ahadi hizo wakati diwani mteule wa kata hiyo, July Sawani akikabidhiwa na wasimamizi wa uchaguzi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa hati yake ya ushindi baada ya kushinda bila kupingwa katika uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika Januari 13, mwaka huu.

Aliahidi mambo hayo matatu baada ya diwani mteule wa kata hiyo kuzungumzia kero mbalimbali za maendeleo na mikakati yake atakayotumia kuzishughulikia.

“Moja ya kazi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ni kusimamamia utekelezaji wa Ilani ya CCM. Ilani hii inazungumza maendeleo ya watu. Na kwa kuwa halmashuri zetu hazina mapato ya kushughulikia kero zake zote, zinahitaji ufadhili na michango ya kila mwenye nafasi,” alisema.

Alisema kata ya Kihesa anayoijua yeye ni ile yenye vijana wengi wasio na ajira ambao kwa bahati mbaya wamekuwa wakishughulishwa kwenye siasa badala ya kuhamasishwa kufanya shughuli za maendeleo.

Alisema vijembe na malumbano ya kisiasa katika kata hiyo yanatosha na akawataka vijana hao kuunda vikundi vya ujasiriamali vitakavyowawezesha kufikiwa kirahisi na mipango mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake diwani mteule wa kata hiyo aliahidi kutumia mfuko wake binafsi kukarabati barabara ya  Mafifi kwasababu imekuwa kero kubwa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

“Kazi hii itaanza wiki hii na sio kwa kutumia greda la manispaa, hapana, nitatufuta greda lingine kwa gharama zangu na litaifanya kazi hiyo kuanzia wiki hii,” alisema.

Sawani alizungumzia pia namna wananchi wa kata hiyo wanavyotakiwa kujiondoa na umasikini kwa kufanya kazi yoyote halali na kwa bidii huku akiasa kwamba hakuna kiongozi wa kisiasa wakiwemo madiwani wanaochaguliwa kwa lengo la kugawa fedha kwa wananchi.

“Kuweni na ndoto za kuondokana na umasikini na zitumie ndoto hizo kuja na mikakati na mipango itakayowaondoka katika hatua moja kwenda nyingine ya mafanikio,” alisema.

Sawani aliwashukuru wana CCM, wananchi wa kata hiyo na vyama vingine vya siasa ambavyo kwa heshima yake alisema havikusimamisha wagombea na kumfanya apitwe bila kupingwa.

“Kwa heshima hiyo najiona nina deni kubwa sana kwa wananchi wa kata hii, niombe ushirikiano kutoka kwenu kwasababu mchakato wa maendeleo unaohusisha nguvu zetu wote,” alisema.


Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali, wabunge na wapenzi wa chama hicho, Asas aliwapokea wanachama wapya 53 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuwakabidhi kadi za chama chake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment