Monday, 18 December 2017

VYAMA SITA VYA UPINZANI VYASUSIA UCHAGUZI MDOGO WA JANUARI 13

Image result for vyama vya upinzani

Siku 26 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu nchini, vyama sita vya upinzani vimesema havitashiriki kutokana na mazingira ya ushindani kutokuwa sawa.

Wakati Kiongozi wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe akithibitisha kutoshiriki kwa chama hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokea wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 , vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) navyo havitashiriki.

Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kupitia mkutano uliovihusisha vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chaumma ambacho kilialikwa, havitashiriki uchaguzi huo hadi vitakapokutana na NEC na kujadiliana.

Mbowe alibainisha kuwa kutokana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa kata hizo, vyama hivyo, NEC na Serikali vilipaswa kukaa katika meza ya majadiliano, kusitisha uchaguzi wa ubunge uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani ili wadau wakutane kufanya tathmini ya changamoto zilizojitokeza.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Zitto aliilalamikia Serikali kwa kuwakandamiza wapinzani na kutumia vyombo vyake kuwadhibiti ikiwa ni pamoja na kuwakamata viongozi wa kisiasa na kuwaweka ndani mawakala wa vyama vya upinzani.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment