Monday, 4 December 2017

TBS YATAKA WENYE VIWANDA MKOANI IRINGA KUTHIBITISHA UBORA
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa rai kwa wazalishaji wenye viwanda mkoani Iringa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kulinda afya za watumiaji na kukuza masoko yao.

Akizungumza na wanahabari juzi, Afisa Masoko wa TBS, Rhoda Mayugu alisema TBS imejipanga kudhibiti bidhaa zisizo na ubora katika maeneo yote nchini.

Muyugu aliyekuwa mjini Iringa akishiriki michuano inayohusisha wafanyakazi wa mashirika ya umma, kampuni za watu binafsi na taasisi mbalimbali (SHIMUTA) aliupongeza mkoa wa Iringa akisema ni mmoja kati ya mikoa yenye viwanda vingi ambavyo malighafi zake zinatokana na bidhaa za kilimo

Alisema upimaji wa ubora wa bidhaa huzingatia mazingira ya uzalishaji, maelekezo ya uzalishaji yaliyoainishwa ndani ya kiwango cha bidhaa husika, kifungashio kilichokusudiwa na maelezo sahihi kwenye lebo ya bidhaa.

Ili kudhibiti ubora wa bidhaa hizo, alisema TBS inatoa leseni za matumzi ya alama ya ubora kwa bidhaa zilizokidhi viwango stahili kila baada ya mwaka mmoja.

“Kupata leseni hii mzalishaji anatakiwa kulipia, lakini TBS inatoa msamaha wa miaka mitatu kwa wazalishaji wadogo na wakati,” alisema huku akiwakumbusha wazalishaji kutofautisha kati ya nembo ya TBS na alama ya ubora.

“Ni muhimu wazalishaji wakatofautisha kati ya nembo ya TBS na alama ya ubora, hii ni kutokana na baadhi ya wazalishaji kuweka nembo ya shirika kwenye bidhaa zao badala ya alama ya ubora,” alisema.

Aidha alisema TBS imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara viwandani na masokoni ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kusambazwa ni zile ambazo viwango vyake vimethibitishwa na TBS.

“Ukaguzi huu ni wa kushtukiza, tunaufanya viwandani na sokoni. Na hufanyika mara nne kwa mwaka au zaidi ya hapo pale inapobidi,” alisema.


Kwa wazalishaji wa bidhaa za vyakula, alisema wanatakiwa kupata kwanza leseni ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kabla ya kupata leseni ya TBS.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment