Monday, 18 December 2017

TANZANIA YAPINGWA KUGOMBEA USPIKA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI

Image result for bunge la afrika mashariki

Uchaguzi wa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) ambao ulikua ufanyike leo umesogezwa hadi kesho kupisha mashauriano yatakayofanywa na baraza la mawaziri wanachama wanaohusika moja kwa moja na Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) baada ya mbunge kutoka Uganda, Freddy Mbidde kupinga Tanzania kuwa na mgombea.

Chanzo cha mgogoro huo kinadaiwa ni Tanzania kuwa na mgombea wa nafasi ya Uspika, Adam Kimbisa wakati nafasi hiyo huwa ni kupokezana na Spika wa kwanza wa Eala, Abdulrahman Kinana alitoka Tanzania akifuatiwa na Kenya kisha Uganda.

Mbidde ametoa hoja ya kuahirishwa kwa bunge kutokana na akidi kutotimia wakati wa kufanya uchaguzi licha ya wabunge kutoka nchi zote sita kula kiapo cha utii mbele ya Katibu wa Bunge hilo, Kenneth Madete.

Baadaye ilibainika wabunge wengi wa Tanzania na Burundi hawakuwemo kwenye ukumbi wa bunge na Mbidde kuomba kutoa muda wa mashauriano zaidi ili kuruhusu nchi zinazostahili kuwa na wagombea kufanya hivyo ambazo ni Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.

Hata hivyo hadi jana wagombea wa nafasi hiyo walikua watatu ambao ni Adam Kimbisa, Leontine Nzeyimana ambaye ni Waziri wa zamani Afrika Mashariki wa Burundi na Mwendesha mashtaka Mkuu mstaafu wa Rwanda, Dk Martin Ngoga huku Sudani Kusini ambaye ni mwanachama mpya katika jumuiya hiyo haikutoa mgombea.

Katibu wa Bunge, Kenneth Madete ameahirisha bunge hadi kesho saa 8:30 mchana kwaajili ya kumchagua Spika na baadaye makamishna na kuunda kamati mbalimbali zitakazosaidia kutekeleza majukumu ya bunge hilo la nne.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dk Suzane Kolimba amekiri kuwa baraza la mawaziri watakutana kushauriana ni njia ipi itumike kabla ya uchaguzi wa kumpata Spika wa nne.

"Kumetokea kutokuelewana na sisi baraza la mawaziri tutakutana kushaurina namna ya kusonga mbele katika hali hii na uchaguzi utafanyika kama mnavyojua suala la akidi ni muhimu katika vikao vya wabunge," amesema Kolimba

Awali wabunge tisa kutoka nchi sita wanachama wa EAC ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini waliapa kuwa wabunge katika kipindi cha miaka mitano ijayo.


Katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa bunge la Tanzania, Azzan Musa Zungu amemwakilisha Spika wa Bunge, Job Ndugai pia walikuwepo Spika wa bunge la Senate la Kenya, Ken Lusaka Spika wabunge la Senate ya Rwanda, Banard Mukuza, Spika wa bunge la Sudani Kusini, Anthony Makana.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment