Sunday, 3 December 2017

RC MASENZA AZUNGUMZIA POMBE YA ULANZI INAVYOATHIRI JAMII

Image result for pombe ya ulanzi
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ameiponda pombe ya kienyeji aina ya Ulanzi wakati akiwataka wakazi wa mkoa huo ambao ni mmoja kati ya mikoa inayoongoza kwa matumizi ya vinywaji vyenye kilevi nchini kupunguza matumizi yake akisema madhara yake yanatisha.

“Wanaokunywa ulanzi wanasema unawapa shibe, lakini taarifa za kitabibu zinaonesha jinsi pombe hiyo ilivyo na madhara makubwa mwilini,” alisema juzi mjini Iringa wakati akifungua kongamano lililojadili changamoto zitokanazo na pombe.

Kongamano hilo liliandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Vijana, Walio Katika Mazingira Magumu na Uangalizi wa Mtoto (IDYDC) kupitia mradi wake wa mapambano dhidi ya unywaji wa pombe uliokithiri unaofadhiliwa na Shirika la IOGT-NTO Movement la Sweden.

Akizungumzia madhara ya kiafya Masenza alisema ulanzi unaathiri utumbo, unaleta ukondefu, uharibu vinywa na meno na huwafanya baadhi ya watoto waonekane na utapiamlo.

Kama ilivyo kwa pombe zingine zikiwemo zile za viwandani, alisema ulanzi nao hupunguza nguvu kazi, huwaingiza watu wengi katika migogoro ya ndoa, ngono zembe na  imekuwa kichochoea cha vitendo vya ubakaji na ulawiti katika maeneo mbalimbali hali inayosababisha pia baadhi ya wanafunzi wakatishe masomo yao.

Kwa upande mwingine alisema anatambua faida itokanayo na biashara ya pombe kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, lakini akaonya “hii isiwe kisingizio cha kunywa kupita kiasi.”

Katika kukabiliana na changamoto za pombe alisema ipo haja kwa mamlaka zinazohusika na utoaji wa leseni kuangalia upya maeneo yanayoruhusiwa kwa biashara hizo, kusimamia sheria, na kushirikiana na wadau kutoa elimu ya kupunguza matumizi yake.

Awali Mkurugenzi wa IDYDC, John Mkoma alisema matumizi ya pombe mkoani Iringa ni makubwa kuliko ya dawa za kulevya.

Kwa kupitia mradi wao wa kukabiliana na changamoto za pombe unaotekelezwa Iringa Vijijini, alisema asilimia 41.9 ya watu wazima na 36.3 ya watoto waliohojiwa walikiri kutumia pombe.

Mkoma alisema sehemu kubwa ya watu wanaotumia pombe Iringa Vijijini hawaoni kama zina madhara kwao kwani wamekuwa wakizinywa kama kiburudisho.

“Bahati mbaya wengi wao wanakunywa pombe za kienyeji, zisizo na kiwango cha ubora, zilizochakachuliwa na kwa kutiwa dawa mbalimbali ili kuongeza ukali wake. Kwahiyo tumeona tuishirikishe jamii ili iyaone madhara yake,” alisema.

Kwa kupitia kongamano hilo wadau mbalimbali walijadili madhara ya pombe kiafya, kijamii na kiuchumi, uhusiano na magonjwa yasiyoambukizwa na pombe na wakachambua sheria na utekelezaji wake pamoja na kufanya mdahalo kuhusu mipango ya idara ya afya, Polisi, ustawi wa jamii, biashara na elimu katika kukabiliana na matumizi hatarishi 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment