Friday, 15 December 2017

RC MASENZA AWAVALIA NJUGA WADAIWA SUGU WA SACCOS YA WALIMU

MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ametoa siku saba kwa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Walimu wa Manispaa ya Iringa (IMTS)  kuamua namna kitakavyokusanya Sh Milioni  175 wanazodaiwa wadaiwa wake sugu.

Mmoja kati ya wadaiwa 166 wa Saccos hiyo ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa inayodaiwa Sh Milioni 3.6 zilizokopwa kuongezea kiasi cha fedha kilichotumika kununua gari kwa ajili ya matumizi ya mstahiki meya wa manispaa hiyo.

Akifungua mkutano wa Saccos hiyo juzi, Masenza alisema ili kukinusuru chama hicho na hatari ya kufa kutokana na madeni hayo kina njia tatu za kufanya kusaidia kurejesha fedha zake.

Alizitaja njia hizo kuwa ni pamoja na kuwaita wadaiwa wote sugu na kukaa nao katika meza ya maridhiano ya namna ya kulipa madeni yao, au kuwatumia wakusanya madeni kudai fedha hizo na kuwapeleka mahakamani wadaiwa wote.

“Inasikitisha kuona ofisi ya mkurugenzi wa manispaa nayo ni mdaiwa sugu wa Saccos hii, namuagiza mkurugenzi wa manispaa kulipa deni hilo haraka iwezekanavyo na kusimamia urejeshaji wa mikopo ya walimu hao kwasababu wengi wao ni waajiriwa wake,” alisema.

Aidha mkuu wa mkoa alizungumzia namna ofisi yake inavyosaidiana na Saccos hiyo kufuatilia kesi ya upotevu wa zaidi ya Sh Milioni 248 inayowakabili wanachama watatu waliowahi kuwa viongozi wake.

“Baada ya kueletewa suala hili nimelifuatilia kwa karibu na kwa umakini mkubwa, niwajulishe tu kwamba kesi hiyo bado ipo kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali ikisubiri maamuzi yake. Hivyo tuwe wavumilivu,” alisema. 

Alisema anataka kuona Saccos hiyo na nyingine zote mkoani Iringa zinaendeshwa kwa faida akitambua namna vyama hivyo vinavyoweza kuwa chachu ya kuchochea ujenzi wa uchumi wa kati, wa viwanda na wa mtu mmoja mmoja.

Awali Mwenyekiti wa Saccos hiyo, Sangiwa Kilonzo alisema pamoja na kudai,  chama hicho kinakabiliwa na madeni makubwa yanayokifanya kionekane kinajiendesha kwa hasara kubwa.

Alisema miongoni mwa wa watu wanaokidai  ni pamoja na walioacha au kujitoa uanachama, waliofariki na wastaafu.

“Wanachama waliojitoa wanadai Sh Milioni 103, waliostaafu wanatudai Sh Milioni 88 na waliofariki walikuwa wakitudai Sh Milioni 9.2 hivyo kufanya deni lote la chama kuwa zaidi ya Sh Milioni 191,” alisema.

Alisema chama hicho chenye wanachama 227 wanaochangia moja kwa moja kutoka katika mishahara yao kina hisa zenye thamani ya Sh Milioni 5.5 baada ya kuondoa hisa zilizowekwa katika mradi wa uwakala wa benki ya CRDB, amana ya Sh Milioni 5.5 na akiba ya Sh Milioni 43.6.

Alisema kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, chama kimeweza kutoa mikopo kwa wanachama wake yenye thamani ya Sh Milioni 89.65 inayotarajiwa kuingiza riba ya Sh Milioni 27.1.

Alitoa wito kwa wanachama wanaokopa kufanya marejesho kwa wakati ili kuleta maendeleo kwenye chama kwa haraka.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment