Tuesday, 5 December 2017

NI CHALAMILA AU BALAMA NA ASAS AU MKINI UCHAGUZI CCM IRINGA

LEO ndio leo katika ukumbi wa Kichangani mjini Iringa pale wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) watakapofanya maamuzi muhimu kuchagua viongozi wao wa mkoa wa Iringa, watakaokiongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, mgombea Albert Chalamila anapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho akipigiwa chapuo na wana CCM wanaounga mkono mabadiliko makubwa ya kimfumo ndani ya chama hicho.

Mgombea mwingine anayepewa nafasi ya kunyakua kiti hicho ni Evans Balama, mkuu wa wilaya mstaafu ambaye pamoja na kupigiwa chapuo na wakongwe ndani ya chama hicho anategemea jukwaa wakati wa uchaguzi huo kubadili upepo unaoonekana kuvuma zaidi kwa Chalamila.

Mgombea Daniel ambaye hatajwitajwi sana katika kinyang’anyiro hicho anaelezwa na wafuatiliaji wa uchaguzi huo kutegemea maajaliwa ya Mwenyezi Mungu kushinda uchaguzi huo.

Kinyang’anyiro kinachoonekana rahisi katika uchaguzi huo ni cha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuwakilisha mkoa wa Iringa.

Wafuatiliaji wa uchaguzi huo wanasema hakuna shaka mgombea Salim Abri  Asas atashinda kwa kishindo nafasi hiyo na hivyo kuwaacha kwa kura nyingi Marcelina Mkini na Elias Mbungu.

“Huenda hii kauli wasiipende sana lakini ukweli ni kwamba Salim Asas amekifanyia na anaendelea kukifanyia makubwa chama hiki. Ni mtu mwenye mapenzi ya dhati ambaye siku zote amekuwa hasiti kutoa mchango wake wa hali na mali kukijenga chama hiki,” alisema mpiga kura mmoja wapo.

Mbali na kukijenga chama, Asas anaelezwa namna anavyojitolea kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, ujasiriamali na zingine nyingi, sifa zinazompa nafasi zaidi ya kunyakua kiti hicho.

Katika uchaguzi huo, chama hicho pia kitawapigia kura Mwinyiheri Baraza, Andrew Ghemela na Josia Kifunge wanaowania nafasi moja ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Iringa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment