Friday, 15 December 2017

MKOA WA IRINGA WAZINDUA MPANGO KAZI WA UJENZI WA VIWANDA 100


MKOA wa Iringa umezindua rasmi mpango kazi wake wa ujenzi wa viwanda vipya zaidi ya 100 ifikapo Desemba 2018 huku kila halmashauri ikianisha viwanda vya vipaumbele kwa kuzingatia fursa zilizopo, upatikanaji wa malighafi na uendelevu wake.

Mpango huo umezinduliwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini Iringa ikiwa imeudhuriwa na wakuu wa wilaya, watendaji wa halmashauri na baadhi ya wamiliki wa viwanda.

Akizindua mpango huo, Masenza alisema viwanda hivyo vinaweza kutumia kongani mbalimbali zilizopo kama vile kongani ya alizeti, mpunga, nyanya, soya, viazi mviringi, mahindi, misitu na mifugo.

Alisema kwa kupitia mpango huo kila wilaya kwa kupitia halmashauri zake inatakiwa kujenga viwanda 35 katika kipindi cha mwaka mmoja, huku ujenzi wa viwanda 20 ukitakiwa kukamilika ifikapo Juni, mwakani na vingine 15 ifikapo Desemba mwakani.

Mkoa wa Iringa wenye wilaya tatu za Iringa, Mufindi na Kilolo unaundwa na halmashauri tano ambazo ni pamoja na ya Manispaa ya Iringa, Wilaya ya Iringa, Kilolo, Mufindi na Mafinga Mji.

Alisema utekelezaji wa mpango huo utafanikiwa kwa kutegemea jasho na maarifa ya wana Iringa na wadau wake hivyo ni wajibu wa kila halmashauri kuweka mazingira bora ya ujenzi wa viwanda hivyo bila kukwamisha juhudi za wale wenye nia nzuri ya kuwekeza katika sekta hiyo.

“Pamoja na halmashauri, mamlaka zingine za udhibiti kama vile Shirika la Umeme Tanzania, Mamlaka ya Mapato, Mamlaka ya Maji Safi, Shirika la Viwango, na Mamlaka ya Chakula na Dawa zisaidie kuweka mazingira wezeshi,” alisema.

Alitaja manufaa ya kuanzishwa kwa viwanda hivyo mkoani Iringa kuwa ni pamoja na mazao ya kilimo kupata nafasi ya kusindikwa na hivyo thamani yake kuongezeka na kutoa ajira mpya hasa kwa vijana.

Manufaa mengine ni vitasaidia kuongeza mapato ya serikali na wananchi wake pamoja na fedha za kigeni kwa bidhaa zitakazouzwa nje, kuvutia wawekezaji wakubwa toka nje ya nchi na vitaimarisha huduma na sekta nyingine za maendeleo.

Baada ya uzinduzi huo, Masenza aliagiza kila wilaya kufanya uzinduzi wa namna itakavyotekeleza mipango yake ya ujenzi wa viwanda hivyo.

Alisema kwasasa mkoa wa Iringa una viwanda vikubwa 24, vya kati 35, vidogo 149 na vidogo zaidi 3,000.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment