Wednesday, 6 December 2017

IDARA YA VYUO NA VYUO VIKUU IRINGA YAPATA VIONGOZI WAPYAUMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa unazidi kuimarisha idara zake baada ya hii leo Idara ya Vyuo na Vyuo vya Elimu ya Juu kupata viongozi wake wapya watakaodumu kwa miaka mitatu ijayo.

Mbali na uwezo wa viongozi hao, wapiga kura walizingatia uwakilishi wa vyuo vyote vitatu vya mjini Iringa wakati wakiwachagua; ambavyo ni Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa ambavyo kwa pamoja vina wanafunzi zaidi ya 5,000.

Katika mkutano huo wa uchaguzi, wapiga kura walimchagua Abeid Mhongole wa Chuo Kikuu cha Iringa kuwa Mwenyekiti wa seneti ya idara hiyo na Shaibath Kapingu kuwa Katibu.

Aidha Mkutano huo uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa Kenani Kihongosi na Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi wa Mkoa wa Iringa Mwinyikheri Baraza ulimchagua Hillary Kipingi kuwa Katibu wa Hamasa na Masesa Nyahinga (Mkwawa), Gasto Mushi (RUCU) na Julius Machibya (Mkwawa) kuwa wajumbe.

Akiwapongeza viongozi hao, Kihongosi alisema wana wajibu mkubwa wa kushirikiana na viongozi wengine wa UVCCM na chama hicho kuongeza idadi ya wanachama, hususani wa kike ambao idadi yao katika idara hiyo bado ndogo.

“Lakini pia msiishie kwenye vyuo vikuu pekee, nendeni hadi kwenye vyuo vya kawaida vilivyoko katika wilaya zote za mkoa wa Iringa,” alisema.

Wakati wakifanya kazi hiyo, Kihongosi alionya makundi ndani ya idara na umoja huo, akisema hayana nafasi katika kipindi chote atakachokuwa kiongozi wake.

Pamoja na kukataa makundi, mwenyekiti huyo alisema umoja wake hautafanya kazi kwa maelekezo ya watu wanaotafuta maslai yao binafsi badala ya chama.

“Katika kitu kinachoniudhi ni wale watu ambao siku zote wamekuwa wakijifanya wana maelekezo kutoka juu. Katika uongozi wangu ni kitu kinachoitwa maelekezo ni marufuku, mambo yote yatafanywa kwa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu za umoja na chama,” alisema huku akikataa kupangiwa viongozi na watu wa kufanya nao kazi.

Alisema CCM na jumuiya zake inahitaji makada watiifu, wanaokipenda chama kwa dhati hivyo ni muhimu wafitini, wambea na wazushi wakaogopwa kama ukoma.

Akishukuru kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa seneti ya idara hiyo, Mhongole alisema amepokea maagizo yote na watayafanyia kazi kwa faida ya CCM.


“Lengo letu ni kuona nguvu ya CCM ndani na nje ya vyuo na vyuo kikuu inakuwa kubwa katika kipindi chote tutakachokuwa viongozi wake, na malengo yetu ni kuiwezesha CCM kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment