Friday, 8 December 2017

HII NDIO HOTUBA ILIYOMPA USHINDI WA NEC SALIM ASAS







CCM Oyeeeeee, Nyela Kamwene......Mheshimiwa mwenyekiti wa mkutano huu, Amani Mwamwindi, viongozi mliopo meza kuu, na wajumbe wa mkutano huu wa mkoa.

Niliyesimama mbele yenu naitwa Salim Abri lakini wengi hupenda kuniita Salim Asas.

Ndugu wajumbe mimi ni mzaliwa wa Mkoa wa Iringa manispaa ya Iringa nimekulia hapa hapa Iringa nimesoma hapa hapa Iringa, ndugu zangu mimi ndimuyenu….(kicheko cha shangwe)

Nimejiunga na Chama cha Mapinduzi mwaka 1986, nilipomaliza shule nikajiunga na Chama cha Mapinduzi, tangia wakati huo mpaka sasa nimebaki kuwa mwanachama mwaminifu, mtiifu na msikivu wa chama cha mapinduzi bila kukiasi wala kukisaliti.

Nimesimama mbele yenu naomba nafasi ambayo sikukurupuka kuiomba, nilitafakari nilifikiri, niliona hii nafasi nayoomba kuwa mjumbe wenu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, kwamba nafasi hii naiweza

Kwanini nimeomba nafasi hii?......kutokana na muda siwezi kueleza yote niliyoifanyia Chama cha Mapinduzi tangia kujiunga na chama hiki.

Nimekuwa kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa kwa miaka 10, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM kwa miaka 15, mwanakamati na mweka hazina wa kuchangisha mifuko ya chaguzi za chama toka mwaka 2000 hadi 2015.

2005 niliwekwa kwenye kamati ya ushindi wa CCM Mkoa wa Iringa; mwaka 2005 mkoa wa Iringa ulioongoza kutoa kura za urais kitaifa tulikuwa wa kwanza kitaifa, mimi nilikuwa mmoja wapo wa kusababisha ushindi huo.

Kwahiyo na uwezo wa kushauri chama chetu na katika kikao nitakachohudhuria nahakika nitakuwa na uwezo wa kushauri na kurudisha ushindi huu kitaifa katika mkoa wetu wa Iringa.

Ndugu wajumbe mimi mzigo huu wa kuwa mjumbe wenu nauweza, nipeni mzigo huu wa kubeba matatizo yenu na changamoto zenu na kuzipeleka Halmahsuri Kuu ya Taifa na kuwasemea kwa maslai ya chama

Ndugu wajumbe……unapokuwa na panya anakusumbua nyumbani kwako, unaambiwa utafute Paka, lakini ushauriwi rangi ya Paka (kicheko cha shangwe).

Kuna panya wanasumbua hapa manispaa ambao wanatuletea kadhia (Mbunge na Madiwani wa Chadema), ndugu wajumbe bila kujali rangi ya Paka nipeni kazi hiyo ili niweze kuwaondoa panya hao na kuleta mabadiliko katika manispaa na mkoa wetu.

Ndugu wajumbe kwa heshima na tahadhima naomba kura zenu zote.

Baada ya hotuba yake hiyo, hakukuwa na mjumbe yoyote aliyekuwa na swali la kumuuliza Salim Asas, hata pale mwenyekiti wa mkutano huo Amani Mwamwindi (Meya Mstaafu wa Manispaa ya Iringa) alipouliza tena na tena hapakuwepo mtu aliyejitokeza kuuliza swali.

Kisha Salim aliyekuwa mgombea wa kwanza kujieleza katika jukwaa la mkutano huo akashuka taratibu na kuelekezwa sehemu ya kukaa, nje ya ukumbi ili kupisha wagombea wengine wawili wa nafasi hiyo nao wajieleze.

Katika kinyangiro hicho Salim Asas alipata ushindi wa kimbunga kwa kuzoa kura 502 kati ya kura 591 zilizopigwa.


Mgombea aliyemfuata Marcelina Mkini alipata kura 74 na Benard Mbungu kura 15. Kwa pamoja wagombea hawa likubali kushindwa na kuahidi kutoa ushirikiano wa viongozi wote waliochaguliwa

Reactions:

0 comments:

Post a Comment