Sunday, 3 December 2017

DC ASIA ABDALLAH ACHANGIA UJENZI WA SEKONDARI YA NYANZWA
MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah amechangia mifuko 50 ya sementi na bati 30 zitakazosaidia kukamilisha miundombinu ya awali ya shule ya sekondari ya kata ya Nyanzwa inayotarajiwa kuanza kutoa huduma hiyo mepema mwakani.

Shule hiyo inayoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo wa wilaya hiyo inahitaji vyumba nane vya madarasa, ofisi ya walimu na mkuu wa shule, vyoo na miundombinu mingine muhimu ili ianze kupokea wanafunzi.

Wakati akishukuru kwa msaada wa mkuu wa wilaya, diwani wa kata hiyo, Amidu Kilamba alisema wanafunzi wa kata hiyo wanaochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, wanasoma katika shule ya Mtandika ambako ni zaidi ya kilometa 40 kutoka katika kata hiyo.

“Huko Mtandika baadhi yao wanaishi katika hosteli za shule ambazo hazikidhi mahitaji ya wanafunzi wote, lakini wengine wamepanga katika nyumba za wenyeji jambo linaloweza kuzorotesha maendeleo ya taaluma yao kwasababu ya kukosa waangalizi wa karibu,” alisema.

Akichangia vifaa hivyo vya ujenzi vitakavyokabidhiwa hivi karibuni kwa kamati ya ujenzi wa shule hiyo, mkuu wa wilaya alisema; “Kukamilika kwa shule hii kutasaidia kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaostahili kujiunga na sekondari kutokana na ongezeko la ufaulu.”

Aliitaka kamati ya ujenzi wa shule hiyo iliyo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na vyoo kuongeza kasi ya ujenzi wa ofisi ya walimu na mkuu wa shule.

“Nimekagua vyoo vya wanafunzi na walimu, madarasa na ofisi ya walimu na mkuu wa shule, mnatakiwa kuboresha baadhi ya miundombinu ya majengo hayo na hadi Desemba 15 ujenzi uwe umakamilika” alisema.

Kwa upande wa wananchi, DC Abdallah aliwaomba waendelee kuchangia nguvu kazi yao akisema yote hiyo ni kwa faida ya vijana wao wanaolazimika kusoma mbali kwasababu ya ukosefu wa shule ya sekondari katika kata yao.


Wananchi wa kata hiyo waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kamati ya ujenzi wa shule hiyo wakisema hatua hiyo itawanusuru watoto wao wanaowahofia usalama wao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment