Tuesday, 5 December 2017

ASAS, CHALAMILA WAIBUKA KIDEDEA, WAAHIDI KUKOMBOA JIMBO LA IRINGA MJINI

KAMA ilivyotarajiwa, Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa leo kimemchagua Albert Chalamila kuwa mwenyekiti wake na Salim Abri Asas kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM huku wote wakiahidi kukomboa jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Pamoja na kukomboa jimbo hilo linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kwa awamu ya pili sasa (toka 2010), viongozi hao wapya wameahidi pia kukiwezesha chama hicho kushinda kwa kishindo uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kihesa, utakaofanyika Januari, mwakani, na kukomboa halmashauri ya manispaa ya Iringa kutoka mikononi mwa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Chalamila anayependa kuitwa Mwalimu ni Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo) na Asas ni mkurugenzi wa kampuni za ASAS zinazojishughulisha na usafirishaji, ufugaji, viwanda, biashara ya mafuta na majengo ya kupangisha.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi uchaguzi huo Januari Makamba alisema mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 617.

Makamba ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alisema mkutano huo ulimchagua Chalamila kuwa mwenyekiti wake kwa kumpa kura 523 dhidi ya kura 61 alizopata mpinzani wake mkuu wa wilaya mstaafu, Evans Balama na kura 9 alizopata Daniel Kidava.

Kwa upande wa mjumbe wa NEC, Salim Asas alishinda kwa kuzoa kura 502 dhidi ya kura 74 alizopata Marcelina Mkini na 15 alizopata Benard Mbungu.

Aidha mkutano huo uliwachagua Dickens Lulanda na Rita Mlagala kuwa wajumbe wa Halmashauri ya CCM Mkoa wa Iringa kutoka Iringa Vijijini.

Wakati Lulanda alipata kura 311, Mlagala alipata kura 308 dhidi ya kura 261 alizopata Augustino Gwelino, 131 za Daniel Chota, 112 za Joshua Nyagawa na 89 alizopata Lediana Mng’ong’o ambaye hata hivyo alitangaza mapema kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa upande wa wilaya ya Mufindi, mkutano huo ulimchagua Gerald Kahemela (343) na Donald Kalima (373) kuwa wajumbe wa halmashauri hiyo ya mkoa baada ya kuwashinda Juma Fulgens (108) na Brastus Mgimwa (174).

Kutoka Iringa Mjini,  Vitus Mushi aliyepata kura 297 na  Zainabu Mwamwindi aliyepata kura 202 walichaguliwa kuwa wajumbe wa kikao hicho baada ya kuwabwaga Maxmillan Lugenge aliyejipatia kura 143, Kaijage Kitunzi aliyepata 119 na Kondo Ramadhani aliyeambulia 103.

Na kutoka Kilolo mkutano huo ulimchagua  Leah Mwamoto  kwa kura 324 na Joseph Muhumba aliyepata kura 322 kuwa wajumbe wa kikao hicho baada ya kuwabwaga Gervas Kahemela (54), Hilda Mwogofi (114), Mari Sauge (126) na Nancy Nyalusi (179).

Baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Christopher Magala kwa kushauriana na mwenyekiti wake mpya waliitisha kikao maalumu cha halmashauri kuu ya mkoa kilichofanya kazi ya kumchagua Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho.

Kwenye kikao hicho, Mwinyikheri Baraza alichaguliwa kuwa Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa katika kinyang’anyiro kilichowashirikisha wagombea wengine wawili akiwemo Andrew Ghemela na Josia Kifunge.

Akiwashukuru wapiga kura kwa ushindi huo mzito, Chalamila alisema cheche zake ataanza kuzionesha kupitia uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kihesa huku akipiga marufuku majungu, fitina, chuki, umbea na uzushi akisema mambo hayo yamekilemaza chama hicho kwa muda mrefu na kusababisha migawanyiko isiyo ya lazima.

Aidha amesema uongozi wake unataka kuanza majukumu yake ukiwa na mikono safi kwahiyo watakachofanya pamoja na mambo mengine ni kufanya uhakiki wa mali zote za chama na jumuiya zake ili kujua namna zinavyotumika na kukisaidia chama hicho.

Naye Salim Asas alisema mkoa wa Iringa ni mkoa ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiongoza kwa kutoa kura nyingi kwa wagombea wa ngazi mbalimbali za uongozi.

Akijifananisha na Paka alisema anatambua uwepo wa panya (wapinzani) katika Jimbo la  Iringa mjini na sehemu kadhaa katika mkoa huo,  hivyo moja ya jukumu lake litakuwa ni kusaidiana na wana CCM wenzake kuwafukuza panya hao ili Jimbo na Kata zote zinazoongozwa na wapinzani zirudi CCM.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment