Sunday, 5 November 2017

WAPIGA KURA KITWIRU WAOMBWA KUMFARIJI LISSU KWA KUINYIMA KURA CCM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wapiga kura wa kata 43 zinazofanya uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani, kuwachagua wagombea wao kama ishara ya kumfariji Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyeko kwenye matibabu nchini Kenya.

Jina la mbunge huyo aliyemiminiwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana wakati akitoka kwenye kikao cha bunge mjini Dodoma hivikaribuni, lilitajwa zaidi ya mara 30 jana na makamanda wa chama hicho waliopanda jukwaani kumnadi mgombea udiwani wa kata ya Kitwiru mjini Iringa anayepeperusha bendera kupitia chama hicho, Bahati Chengula.

Baadhi ya makamanda hao ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu na Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche.

Akiwaomba wapiga kura wa kata hiyo kumchagua Chengula, Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Msigwa alisema itakuwa faraja pekee ya kuponya majeraha ya Lissu endapo wananchi wa kata hiyo watahakikisha mgombea huyo wa Chadema anashinda.

Mchungaji Msigwa alisema huko aliko, Lissu anafuatilia kwa karibu chaguzi ndogo zinazoendelea na wanaamini maumivu yake yatapungua zaidi endapo wagombea wa chama hicho, akiwemo wa kata ya Kitwiru watapata ushindi dhidi ya wagombea wa vyama vingine kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM).

 “Novemba 26 ni siku ya kutuma ujumbe kwa serikali kwamba kuna mambo yanaendelea na hatukubaliani nayo. Ndugu zangu, mama zangu, kaka zangu, na dada zangu ikifika tarehe hiyo amka asubuhi na mapema, kunja ngumi kama ishara ya mabadiliko kisha elekea katika kituo chako cha kupiga kura huku ukimuombea Tundu Lissu halafu piga kura ya kumng’oa kigeugeu aliyekimbilia CCM,” alisema.

Msigwa alisema kuwa watu wamekuwa waoga na wenye hofu katika nchi yao na hata muhimili wa Bunge umekuwa ukiingiliwa na ndio maana anataka kupeleka muswada bungeni wa kutokuwa na imani na Spika Job Ndugai.

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Vijijini alisema alipokuwa Jijini Nairobi kmjulia Tundu Lissu hali, ujumbe aliopewa kwa ajili ya watanzania ni kuwachagua madiwani na wabunge kutoka Chadema katika uchaguzi wowote mdogo utakaofanyika.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini alisema baadhi ya madiwani wa Chadema wanaojiengua katika nafasi hizo na kukimbilia CCM wamekuwa wakinunuliwa jambo ambalo ni ufujaji wa fedha zinazoweza kutumika kwa shughuli zingine za maendeleo.

Akiomba kura, Chengula aliwaambia wananchi wa kata hiyo kwamba ana hali kubwa ya kuwatumikia wananchi wa kata hiyo baada ya kukimbiwa na Baraka Kimata aliyekuwa diwani wao kupitia Chadema kabla ya uchaguzi huo.

Kimata anayegombea kwa mara nyingine nafasi hiyo kupitia CCM alijitoa Chadema hivikaribuni kwa kile alichodai chama hicho cha demokrasia kinaongoza kwa kukandamiza demokrasia.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment