Wednesday, 29 November 2017

UV-CCM MKOA WA IRINGA WAMPA HATI YA PONGEZI SALIM ASAS


KAMANDA wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV-CCM) Mkoa wa Iringa anayemaliza muda wake, Salim Abri (Asas) amepewa hati maalumu ya pongezi kwa kazi na jitihada kubwa alizofanya kuijenga jumuiya hiyo kwa kipindi chote alichokuwa na wadhifa huo .

Amekabidhiwa hati hiyo ofisini kwake mjini Iringa hii leo baada ya jumuiya hiyo mkoa wa Iringa kufanya Uchaguzi na kupata safu mpya ya viongozi wake.

Katika uchaguzi huo, Kenani Kihongosi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa UVCCM akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Tumaini Msowoya, miaka mitatu iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na umoja huo imesema ASAS atakumbukwa kwa namna alivyojitolea kusaidia shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo, vijana wa CCM, na wapenzi wa chama hicho akiwa Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa.

Wakati akimaliza muda wa uongozi huo, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika Novemba 21, 2017 chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk John Magufuli kilimteua Asas kuwa mmoja kati ya wagombea watatu, wanaowania Ujumbe wa NEC Taifa kuwakilisha mkoa wa Iringa.

Wengine walioteuliwa katika kikao hicho ni pamoja na Bernard Elias Mbungu na Marcelina Mkini.

Aidha NEC imewateua Albert Chalamila,  Evans Balama  na Daniel Kidava kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Dk Jesca Msambatavangu aliyefukuzwa uanachama wa chama hicho baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kwa upande wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Iringa, NEC imewateua Mwinyiheri Baraza, Andrew Ghemela na Josia Kifunge kuwani nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Dk Yahaya Msigwa ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Uchaguzi wa CCM Mkoa wa Iringa unatarajia kufanyika mapema wiki ijayo ambapo nafasi hizo zitajazwa pamoja na nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment