Tuesday, 21 November 2017

TRA, DC IRINGA WABAINI MBINU ZINAZOTUMIKA KUKWEPA KODI

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela wamebaini mbinu mpya zinazotumiwa na wafanyabiashara wa mjini Iringa kukwepa kodi kwa kutumia mashine ya risiti ya kielekroniki (EFD).

Katika operesheni ya kushtukiza iliyofanywa  mjini Iringa hivikaribuni, imebainika baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanatoa risiti za kiwango cha chini tofauti na kile kilicholipwa na mteja, na wamekuwa wakitumia risiti ya bidhaa moja kuhalalisha manunuzi ya bidhaa zaidi ya moja.

“Kwa mfano tumekamata Televisheni saba zilizoagizwa na mfanyabiashara mmoja toka Dar es Salaam kwa risiti moja tu ya Sh 80,000, hii inaashiria kuna bidhaa nyingi sana zinasafirishwa kwa mtindo huo na hivyo kuikosesha serikali mapato,” alisema Kasesela.

Akizungumza na wanahabari wakati oparesheni hiyo ikiendelea, Kasesela alitaja udanganyifu mwingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kufanya biashara bila kuwa na namba ya mlipa kodi (Tin Number), wengine hawana mashine za EFD kabisa huku baadhi ya wafanyabiashara hao wakikutwa na mashine zilizoharibika huku wanaotumia wakikwepa kuingiza taarifa zote za mauzo.

“Lakini kuna wengine wana miliki duka zaidi ya moja kwa kutumia majina ya watu wengine na wanafanya hivyo ili kupunguza ukubwa wa biashara ili wakwepe kulipa kodi stahiki serikalini,” alisema.

Alisema katika oparesheni hiyo wamefunga baadhi ya maduka ya wafanyabishara wasio na Tin Number huku akiwataka wafanyabiashara wengine wenye changamoto za aina hiyo kujisafisha ili wasiingie matatani..

“Nikiwa kama msimamizi wa shughuli za maendeleo za wilaya hii nitaendelea kushirikiana na mamlaka zote za serikali ikiwemo TRA kuhakikisha michezo hii inayoikosesha serikali mapato yake inakwisha,” alisema.

Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Lamson Tulyanje alisema  TRA itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa matumizi ya mashine hizo ili kubaini kama kuna mianya ya ukwepaji wa kodi.

“Niwapongeze wafanyabiashara wengi kwa kununua mashine hizo, lakini suala la kununua ni moja na kuzitumia kwa kila kinachouzwa ni lingine. Woti wangu wafanyabishara watoe risiti na wanunuzi wadai risiti,” alisema.


Alisema kwa mujibu wa sheria, anayeshindwa kutoa risiti na anayenunuaa bidhaa bila kuchukua risiti yake, wote wana makosa ambayo faini yake ni hasara kwao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment