Monday, 6 November 2017

SPANEST CUP YANOGA, TUNGAMALENGA WAWEKA MPIRA KWAPANI, KITISI YAZIDI KUDODA


KOMBE la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo limeendelea juzi na jana katika viwanja mbalimbali vya Tarafa ya Idodi na Pawaga huku Mahuninga FC wakijiokotea point tatu za chee baada ya Makifu FC kutotokea uwanjani.

Nayo mechi kati ya Tungamalenga FC na Mapogolo FC haikuweza kuendelea kipindi cha  pili baada ya Tungamalenga kutaka kutumia wachezaji mamluki.

Mabingwa watetezi wa kombe hilo Kitisi FC wamezidi kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa huo kwa mara nyingine tena baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Idodi FC.Magoli ya Idodi FC yalifungwa na Sharifu Gembe.

Nao Nyamahana FC walimbamiza mabao 2-1 Mafuruto FC, magoli yote yakifungwa Said Kifanya. Mafuruto FC walipata goli baada ya mlinzi wa Nyamahana FC Teo Mbembe kujifunga.

Nao Mbaliboli FC na Mbugani FC walilazimisha sare ya bila kufungana huku Ilolompya na Luganga wakitoka sare ya 1-1.

 Nao Kimande FC walipata pointi tatu muhimu baada ya kumbamiza Mbuyuni FC kwa mabao 2-0, mabao yalifungwa na Bahati Malenda na Rashid Mwambungu huku Kinyika FC ikionesha ubabe kwa kuichapa Kisanga FC kwa mabao 3-1, mabao yaliyofungwa na Tizo Nzalamoto.

Ligi hiyo iliyoanza Octoba 21, inaendelea tena kesho Jumamosi katika viwanja mbalimbali vya vijiji hivyo vya wilaya ya Iringa.

Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na cheti, medali na Sh 500,000.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment