Wednesday, 8 November 2017

SPANEST CUP YAINGIA ROBO FAINALI, MABINGWA WATETEZI WATUPWA NJE

MABINGWA watetezi wa Kombe la Spanest Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo, Kitisi FC wameshindwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kupoteza mechi tatu kati ya sita ilizocheza katika hatua ya awali ya ligi hiyo.

Katika hatua hiyo ya awali Kitisi ilipoteza pointi tisa muhimu baada ya kukubali kipigo cha magoli 4-0 kutoka kwa Tungamalenga FC,  4-0 kutoka kwa Mapogolo FC na 2-1 kutoka kwa Idodi FC.

Katika hatua hiyo Kitisi wamemaliza wakiwa na Pointi 4 baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Mapogolo , na kutoa sare Idodi na Tungamalenga.

Mratibu wa Spanest, Godwell Ole Meing’ataki alisema timu sita kati ya 24 zilizoshiriki hatua hiyo ya awali ya makundi zimefanikiwa kuingia nusu fainali itakayoanza kutimu vumbi Jumamosi, katika viwanja mbalimbali vya tarafa ya Idodi na Pawaga, Iringa Vijijini.

Alizitaja timu hizo kuwa ni Kinyika, Itunundu na Ilolompya kwa upande wa tarafa ya Idodi na Mapogolo, Mahuninga na Idodi kwa upande wa tarafa ya Pawaga.

Alisema timu hizo zitaungana na mshindi kati ya Mboliboli na Mkumbwanyi, na Malizanga na Mafuruto ambao mechi zao zinachezwa leo ili kufanya timu shiriki katika hatua hiyo ya robo fainali kufikia nane.

Alisema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.

Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.


Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na cheti, medali na Sh 500,000.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment