Wednesday, 15 November 2017

SOS YATUMIA MILIONI 51 KUBORESHA ELIMU IRINGA VIJIJINI
SHIRIKA la SOS Childrens Village Tanzania limetoa msaada wa vifaa vya ujenzi na vya kufundishia vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 51 milioni kwa shule nane za halmashauri ya wilaya ya Iringa, Iringa vijijini.

Msaada huo umetekelezwa kupitia mradi wao unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia, kuwawezesha watoto walio katika mazingira magumu kupata elimu sawa na kuhakikisha jamii na serikali inaipa kipaumbele haki ya elimu na inaweka bajeti rafiki kwa mtoto.

Mratibu wa mradi huo, Anastazia Lukomo alisema mradi huo unatekelezwa katika wilaya mbalimbali nchini na kwa wilaya ya Iringa unatekelezwa katika kata tatu za Nyang’oro, Malenga Makali  na Ulanda.

Alizitaja shule zinazonufaika kuwa ni Holo, Mawindi, Chamdindi na Ikengeza kwa upande wa kata ya Nyang’oro na Iguruba, Makadupa na Isaka katika kata ya Malenga makali na Ulanda na Chamdindi kwa kata ya Ulanda.

“Kwa kupitia msaada huo tumenunua mifuko ya saruji 546 na vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati wa madarasa na ujenzi wa darasa moja katika shule ya Ulanda, madawati 137 na tunatoa vifaa vya kujifunzia, viatu na sare kwa watoto 285 walio katika mazingira magumu,” alisema.

Hadi kukamilika kwake alisema mradi huo wa miaka mitatu unatarajia kuwafikia watoto zaidi ya 3,000 wakiwemo wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Akishukuru kwa msaada huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Robert Masunya alisema utekelezaji wa agizo la  Rais Dk John Pombe Magufuli la kutoa elimu bure limechangia ongezeko la wanafunzi na kuongeza changamoto katika baadhi ya shule.

“Ieleweka kwamba katika kipindi hiki  watu wengi wamejitokeza kupeleka watoto wao shule hata wale ambao awali walishindwa akufanya hivyo, hatua hiyo imechangia kuwapo kwa changamoto ya miundombinu yakiwamo madawati,vyumba vya madarasa na vifaa vya kufundishia,”alisema.


Katika kukabiliana na changamoto hizo, Masunya alisema serikali inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuboresha mazingira ya kutolea elimu na akawaomba wadau wengine kusaidia jitihada hizo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment