Tuesday, 7 November 2017

SHANGINGI LA MSIGWA LAZUA BALAA KAMPENI ZA UDIWANI KITWIRU

Related image

MBUNGE wa Mtera na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Livingstone Lusinde a.k.a Kibajaji amezua gumzo kuhusu gari la kifahari linalotumiwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akisema; “katika mazingira yake binafsi Mchungaji Msigwa asingekuwa na uwezo wa kununua gari hilo.”

Aliyasema hayo juzi wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikizindua kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kitwiru, mjini Iringa.

Katika Uchaguzi huo CCM imemsimamisha Baraka Kimata ambaye awali alikuwa Diwani wa Kata hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chadema wamemsimamisha Bahati Chengula, mfanyabiashara wa usafirishaji.

Kibajaji alisema wakati Mchungaji Msigwa na wabunge wengine wa upinzani wakikataa kuunga mkono kila bajeti ya maendeleo inayowasilishwa bungeni, hali ni tofauti pale linapokuja suala la maslai yao binafsi ambayo pia yamekuwa yakipitishwa na bunge hilo na vyombo vingine vya serikali.

“Serikali ya CCM ndiyo inayopanga stahiki zote za mbunge, mishahara, posho na marupurupu mengine. Hayo yote wamakuwa wakichukua bila kupinga, lakini linapokuja suala la fedha za maendeleo ya wananchi wamekuwa wakikataa na wakati mwingine wakitoka nje ya vikao vya bunge,” alisema.

Alisema Mchungaji Msigwa ameweza kununua shangingi hilo kwa kuwa amekuwa akipokea stahiki zote anazopewa na serikali ya CCM.

“Na si yeye tu hata mimi nisingekuwa na uwezo wa kuwa na gari nalomiliki kama nisingekuwa mbunge ninayelipwa kwa mipango ya serikali ya CCM,” alisema huku akiwataka wapiga kura wa Kitwiru kumchagua Baraka Kimata kwa maendeleo ya kata hiyo.Reactions:

0 comments:

Post a Comment