![]() |
KAMATI ya mashindano ya Kombe la SPANEST
Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo imetupilia mbali malalamiko ya Mafuluto FC dhidi
ya mchezo wake wa jana na Malizanga FC baada ya kutozingatia taratibu za
uwasilishwaji wake.
Mafuluto na Malizanga walimenyanya katika
mchezo huo wakitafuta kufuzu hatua ya robo fainali ya ligi hiyo itakayoanza
kutimua vumbi Jumamosi.
Ilikuwa katika dakika ya 87 ya mchezo,
Mafuluto waliokuwa wakiongoza kwa goli 1-0 waliposusa kuendelea na mchezo huo
baada ya Malizanga FC kupata bao la kusawazisha.
Ili waweze kufuzu katika hatua hiyo
ilikuwa ni lazima kwa Mafuluto FC kushinda mechi hiyo.
Afisa Habari wa Mashindano hayo, Rashid
Msigwa amesema; “Mafuluto walilalamikia goli hilo, wakasusa kuendelea na
mchezo, lakini wakashindwa kuwasilisha malalamiko yao kwa maandishi na hivyo
malalamiko yao yaliyowasilishwa na waamuzi wa mchezo huo kwa mdomo yametupiliwa
mbali.”
Rashid amesema pamoja na mchezo huo
kuvunjika Dk 87, kamati imeamua matokeo yake yabaki kama ilivyo na hivyo kufanya
timu hizo zigawane pointi hatua iliyoibeba Malizanga FC waliofikisha Pointi 6
katika kundi lao dhidi ya Mafuluto waliofikisha Pointi 5.
Kwa hatua hiyo Malizanga inaungana na
Mboliboli FC iliyoichapa Mkumbwanyi FC kwa magoli 3-2 kufuzu katika hatua hiyo
ya robo fainali.
Timu zingine zilizofuzu hatua Kinyika,
Itunundu na Ilolompya kwa upande wa tarafa ya Idodi na Mapogolo, Mahuninga na
Idodi kwa upande wa tarafa ya Pawaga.
Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Maing’ataki
amesema; “baada ya kupata timu nane zilizofuzu hatua hii ya robo fainali, leo
tutakuwa na shughuli ya kugawa vifaa kwa ajili ya timu hizo.”
Alitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na
jezi, mipira na vifaa vingine vitakavyoziwezesha timu hizo kushiriki hatua hiyo
muhimu kuelekea kupata washindi watatu wa ligi hiyo.
Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka
wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa
Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa
vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki
katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.
“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni
kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za
ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa
hizo,” alisema.
Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa
mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh
Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.
Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba,
cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na
cheti, medali na Sh 500,000.
0 comments:
Post a Comment