Monday, 6 November 2017

POLEPOLE, KIBAJAJI WALIVYOSHUHUDIA CHADEMA IRINGA MJINI IKIPASUKAPASUKA
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa chama hicho, Livingstone Lusinde juzi walishuhudia jinsi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa mjini kinavyozidi kumeguka, wakati wakielekea katika uchaguzi mdogo wa udiwani, kata ya Kitwiru Iringa Mjini.

Katika tukio hilo, Diwani wa Kata ya Kihesa Iringa Mjini, Edgar Mgimwa (Chadema) na wanachama wengine sita wa Chadema walikihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Chadema imepata pigo hilo ikiwa ni miezi miwili na kidogo tangu ikimbiwe na madiwani wengine watatu, akiwemo diwani wa kata ya Kitwiru, Baraka Kimata na Leah Mleleu na Husna Daudi ambao ni madiwani wa viti maalumu.

Baada ya kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio wa kata hiyo, Kimata aliyejiunga CCM muda mfupi baadae alishinda kura za maoni na kusimamishwa kwa tiketi ya chama hicho kuwania tena udiwani wa kata hiyo utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu.

Akitetea uamuzi wa CCM kumsimamisha tena Kimata kuwania udiwani katika kata hiyo aliyoiongoza kwa miaka miwili akiwa Chadema, Lusinde alisema; “Kwa kuwa Chadema walisema mtu kwanza, chama baadae ndio maana tumemrudisha Kimata ili tuone unafiki wao.”

Pamoja na kwamba Kimata alijiunga na CCM muda mfupi baada ya kujitoa Chadema, Leah na Husna walipokelewa na Polepole jana katika tukio lililokwenda sambamba na kumpokea diwani wa kata ya Kihesa na wanachama wengine sita wa Chadema wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani wa kata hiyo.

Akiwapokea madiwani na wanachama hao, Polepole alisema mwaka 2015 CCM walifanya kosa la kizembe lililosababisha jimbo la Iringa Mjini liende tena kwa Mchungaji Peter Msigwa na wapoteze halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa wapinzani wao hao.

Katika uchaguzi huo, Mchungaji Msigwa alimshinda kwa mbali Frederick Mwakalebela wa CCM ambayo pia ilipoteza kata 14 kati ya 18 katika uchaguzi wa madiwani.

“Tukiri tulifanya makosa ya kizembe akapata ubunge, lakini leo nimekuja Iringa kumpa ujumbe mzito Mchungaji Msigwa kwamba ajiandae kurudi kanisani akachunge kondoo wa bwana,” alisema.

Alisema siku za Mchungaji Msigwa zinahesabika kwa kuwa watu wa Iringa, wakiwemo madiwani na wanachama wa Chadema wanaorudi CCM wameanza kubaini jinsi wasivyostahili kuongozwa tena na mtu muongo.

“Huyu Mbunge ndiye yule aliyewahi kusema mtu yoyote atakayemuunga mkono Edward Lowassa anastahili kupimwa akili, cha kushangaza baada ya muda mfupi alikuwa mmoja wa viongozi wa Chadema aliyemuunga mkono kiongozi huyo lakini hadi leo, hajaenda kupimwa akili,” alisema.

Aliwapongeza wana Chadema wanaojitoa na kujiunga na CCM akisema wanaridhishwa na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM unaosimamiwa na Rais Dk John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Akizungumza kwa niaba yao, Diwani wa Kihesa alisema hajutii uamuzi wa kujitoa Chadema na kujiunga CCM kwasababu anaridhishwa na jinsi siasa zake zinavyoendeshwa na namna serikali ya awamu ya tano inavyoshughulikia kero mbalimbali za wananchi.

“Kimsingi mimi nilikuwa mwana CCM kabla ya kugombea udiwani katika kata hiyo mwaka 2015, nilifuatwa na Chadema Julai 2015 na kuombwa kugombea, kuna matatizo makubwa ndani ya Chadema, hakuna demokrasia na kimekithiri kwa ubabe, kwahiyo nimeamua kurudi nyumbani,” alisema Mgimwa.

Polepole na Lusinde waliwataka wapiga kura wa kata hiyo kumchagua Kimata kuwa diwani wa kata hiyo wakisema pamoja na uchache wao katika manispaa ya Iringa, wanaangaliwa kwa jicho kubwa na Rais Dk Magufuli na chama kwa ujumla.

 “CCM tunatambua sehemu ya kata hii kuna tatizo la upatikanaji wa maji, lakini pia kuna tatizo la daraja la Kitwiru. Hiyo ni kazi yetu, ipo ndani ya Ilani yetu hivyo tutaziagiza mamlaka zinazohusika ili zishughulikie,” Polepole alisema.

Akiomba kura kwa wananchi wa kata hiyo Kimata alisema kuna kila dalili Mchungaji Msigwa akabaki  pekee yake katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa kuwa hataki kuambiwa ukweli.

“Nilipokuwa Chadema nilikuwa na mvutano mkubwa na wa muda mrefu wa kiutendaji na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini kwasababu ni mtu asiyeambilika, hataki ukweli na anayeamini anajua kila kitu, nilikuwa pia Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo na hii iliniweka katika mazingira magumu sana. Nimevumilia kulinda heshima ya mbunge na chama lakini ikafikaa mwisho nikasema kuvumilia,” alisema.

Alisema baada ya kujitoa Chadema na kujiunga CCM baadhi ya wana Chadema walimtukana sana na akatumia mkutano huo kuwasamehe na kuwaomba kura kwa kuwa rekodi yake ya utendaji wanaijua.


“Yale niliyoanza kuyatekeleza na niliyoyatekeleza nikiwa Chadema mnayajua, nichagueni ili nikayaendeleze na kwa upande huu kasi yake itakuwa kubwa zaidi kwasababu CCM ndiyo yenye serikali,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment