Saturday, 18 November 2017

ILOLOMPYA YAJIWEKA PAGUMU KOMBE SPANEST


TIMU ya Kinyika FC ipo katika nafasi nzuri ya kucheza nusu fainali ya Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo, baada ya kamati ya mashindano hayo kuizawadia Pointi 3 na mabao matatu ya mezani; maamuzi yaliyotolewa baada ya mchezo wake wa robo fainali dhidi ya Ilolompya FC kutochezwa.

Kinyika ilipewa ushindi huo wa mezani ikiwa ni matokeo ya Ilolompya FC kutaka kuchezesha wachezaji wasio na kitambulisho cha mashindano hayo, na kukataa kukaguliwa kwa mara ya pili baada ya kugundulika kuingiza mchezaji asiye na sifa.

Baada ya kamati hiyo kutoa uamuzi huo jana, Ilolompya hawakuchelewa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa huo wa kamati, rufaa itakayosikilizwa keshokutwa, Jumatatu.

Kabla ya kupokea rufaa hiyo, kamati hiyo ilitangaza kuiondoa Ilolompya katika mashindano hayo na kuipa ushindi huo wa mezani Kinyika ambayo kesho ilikuwa icheze na Itunundu FC katika hatua ya nusu fainali.


Mratibu wa SPANEST Godwell Ole Meing’ataki amesema baada ya kupokea rufaa ya Ilolompya, mchezo wa Kinyika na Itunundu hautafanyika kesho kama ilivyotangazwa mpaka rufaa hiyo itakaposikilizwa.

Wakati mzozo huo ukiendelea, Malizanga FC ambao tayari wamekwishakata tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo, wameendelea kupata muda wa kutosha wa kujifua kwa ajili ya mtanange huo, utakaochezwa hivikaribuni katika tarafa ya Idodi.

Malizanga walikata tiketi ya kuingia fainali hizo baada ya kumchapa Mapogolo katika hatua ya nusu fainali.

Mratibu wa SPANEST, amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment