Thursday, 9 November 2017

NANE BORA SPANEST CUP WAWEKWA SAWA KUSAKA FAINALI

TIMU nane zilizofuzu hatua ya robo fainali ya kombe la Spanest, Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo zimepewa jezi mpya zitakazowawezesha kuwa katika sura mpya wakati zikishiriki hatua hiyo inayoanza Jumamosi.

Hafla ya makabidhiano ya jezi hizo yalifanywa leo katika ofisi za Spanest mjini Iringa ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania.

Akikabidhi jezi kwa makapteni wa timu hizo mapema leo, Mratibu wa Spanest Godwell Ole Maing’ataki alisema wakati Mahuninga FC itaikaribisha Mapogolo FC, Malizanga FC itakuwa katika uwanja wake wa nyumba ikimenyana na Idodi FC.

Ratiba ya Jumapili itazikutanisha timu ya Mboliboli FC vs Itunundu FC huku washindi wa pili wa kombe hilo mwaka jana Kinyika FC wakimkaribisha katika uwanja wake wa nyumbani Ilolompya FC.

Meinga’taki amesema mechi hizo zitapigwa nyumbani na ugenini na timu nne zitakazoibuka washindi katika hatua hiyo zitaingia nusu fainali itakayopigwa Novemba 15 na 16.

Amesema tarafa ya Idodi itakuwa mwenyeji wa fainali ya ligi hiyo itakayopigwa Jumapili ya Novemba 19 ikitanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu katika uwanja utakaopangwa baadaye.

Meing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazmuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment