Monday, 20 November 2017

MWIGULU NCHEMBA AWATABIRIA MABAYA WAPINZANI WA CCM


WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba ameutabiria mabaya upinzani wa kisiasa nchini, akisema umeanza kufa polepole.

Nchemba aliyasema hayo jana wakati akimnadi mgombea mgombea udiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kata ya Kimala wilayani Kilolo mkoani Iringa, Amoni Kikoti.

“Kubaki upinzani sasa ni kupoteza muda, nazunguka sana mikoani, wananchi wanamuelewa sana Rais Magufuli, wananchi wanajua dhamira ya serikali na wanauona mwanga mkubwa wa maendeleo” alisema.

Wakati CCM imemsimamisha Kikoti kujaza nafasi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo Mejusi Mgeveke (CCM) aliyefariki dunia mapema mwaka huu, Chadema imemsimamisha Tumson Kisoma.

 “Wewe ndiye utakayekuwa mgeni wangu wa kwanza wa kikao kijacho cha bunge. Nataka uje na shida mbalimbali za kata yako, nitakutambulisha kwa wadau mbalimbali wakiwemo mawaziri ili wazichukue na kuzifanyia kazi,” alisema wakati akimnadi mgombea huyo katika kijiji cha Kimala.

Dk Nchemba aliyesimama katika jukwaa la kampeni hizo kama Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema uchaguzi wa kata hiyo ni mwepesi kwa chama chake kwa kuwa unalenga kujaza nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na CCM.

“Nitashangaa sana kama suruali nyeusi iliyotoboka itazibwa kwa kiraka cheupe, katika uchaguzi huu kuwapigia kura wapinzani ni sawa na kupigia kura kivuli,” alisema.

Alisema watanzania wote wanajua serikali iliyopo madarakni ni ya CCM, na sera na mipango inayotekelezwa inatokana na Ilani ya CCM.

“Hatushindani kwa sera tena kwasababu tulishindana 2015 na CCM ikaibuka kidedea, sasa hivi tunatekeleza. Maji, barabara, huduma za afya, elimu, umeme na huduma zote muhimu zinaombwa na wananchi kwa serikali ya CCM,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo Kiliani Myenzi  alimuomba Waziri Nchemba kupeleka kilio chao cha miundombinu ya barabara serikalini ili kifanyiwe kazi.

“Zipo barabara ambazo kupita kwake ni shida, lakini tunaomba kwa kiwango cha lami barabara ya kilometa 35 ya Iringa Kilolo,” alisema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto aliwaambia wapiga kura wa kata hiyo wasiifunge kata hiyo na maendeleo.

“Chagueni mgombea mnayejua ana nafasi nzuri ya kuwasiliana na Dk Magufuli, na huyo si mwingine zaidi ya mgombea wa CCM,” alisema.


Akiomba kura kwa wapiga kura hao, Kikoti alisema anazifahamu changamoto za kata hiyo na yupo tayari kushirikiana na wananchi,  serikali ya CCM na wadau wengine katika kuiletea maendeleo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment