Monday, 20 November 2017

MUGABE MGUU NDANI MGUU NJE

Image result for Robert Mugabe

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameapa kuendelea kuongoza taifa hilo kwa wiki kadhaa, licha ya shinikizo kutolewa kumtaka aachie madaraka.

Akihutubu moja kwa moja kupitia runinga ya taifa jana usiku, Mugabe amesema anapanga kuongoza mkutano mkuu wa chama mwezi Desemba licha ya Kamati Kuu ya chama cha Zanu-PF kuidhinisha hatua ya kumvua uongozi wa chama hicho na kumpatia saa 24 ajiuzulu la sivyo wamuondoe madarakani.

Pamoja na msimamo huo, taarifa ya hivipunde iliyonukuliwa na CNN imedai Mugabe yupo tayari kujiuzulu endapo yeye na mkewe watahakikishiwa kinga ya kudumu na mali zake binafsi zisiharibiwe wakati wa maisha yake yote baada ya kujiuzulu.

Jeshi lilichukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita, huku mzozo kuhusu nani atamrithi ukizidi kutokota baada ya Mugabe kuonekana kupoteza udhibiti wa chama chake.

Mzozo huo wa kisiasa ulianza pale Mugabe alipomfuta kazi makamu wake, Emmerson Mnangagwa wiki mbili zilizopita, hatua iliyolikera jeshi ambalo lilitazama hatua hiyo kama jaribio la kumteua mke wake Grace kuwa makamu wa rais na mwisho kuwa mrithi wake.

Mapema Jumapili, Bw. Mnangagwa alitawazwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha Zanu-PF na mgombea wake wa urais uchaguzi mkuu wa 2018.

Wakati huohuo, Mtandao wa Twitter unaofuatilia taarifa za vyombo vya habari nchini Zimbabwe unaripoti kuwa Kiongozi wa chama tawala Cha ZANU PF anaamini mchakato wa kumshtaki Bwana Mugabe utaendelea kama ilivyopangwa Jumanne , wakati ambapo chama-bunge linatarajiwa kukaa.

Hatua hii ni kama muda uliowekwa wa kujiuzulu kwake ambao ni leo Jumatatu saa sita mchana utakwisha kabla Bwana Mugabe hajajiuzulu Watu wa Zimbabwe walikuwa wanatarajia kusikia Mugabe akijiuzulu kulingana na madai yao.

Baadhi ya wale waliokusanyika kufuatilia hotuba yake kwenye vilabu walinukuliwa wakisema kuwa wamekatishwa tamaa kwa kutojiuzulu kwa Rais Mugabe.

Hata hivyo hali ya imeendelea kuwa tulivu katika maeneo mengi ya Zimbabwe, huku wengi wakiendelea kusubiri mchakato utakaofuata. 

Duru kutoka ndani ya mazungumzo ya hatma ya Mugabe zimedai kuwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 alikuwa amekubali kuondoka madarakani , lakini baadae akabadili mawazo yake Jeshi linatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari Jumatatu asubuhi pamoja na Muungano wa Wapiganaji waliopigania Uhuru wa Zimbabwe

Reactions:

0 comments:

Post a Comment