Sunday, 26 November 2017

MKULIMA WA TANANGOZI ASHINDA PROMOSHENI YA WESTERN UNION


MKULIMA Samwel Ngulika (60) wa kijiji cha Tanangozi, Iringa Vijijini ameshinda kompyuta mpakato kupitia promosheni ya shindano la kutumia huduma ya Western Union inayoendeshwa na Benki ya TPB.

Ngulika alikabidhiwa kompyuta hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh 900,000 juzi kwenye hafla fupi iliyofanyika katika tawi la benki hiyo mjini Iringa.

Akimkabidhi kompyuta hiyo, Meneja wa Benki ya TPB tawi la Iringa, Hassan Mugendi alisema mshindi huyo ni mmoja kati ya washindi wawili waliopata aina hiyo ya kompyuta katika droo ya kwanza iliyofanyika Novemba 16 huku washindi wengine watano wakipata simu za mkononi.

Kwa kupitia promosheni hiyo iliyozunduliwa mapema Oktoba, mwaka huu na itakayodumu hadi Januari mwakani, Mugendi alisema wateja wanaotumia huduma hiyo wanaweza pia kujishindia fedha taslimu.

Akimpongeza mshindi huyo kutoka Iringa, meneja huyo alisema ili uweze kushiriki kwenye promosheni hiyo, mteja anatakiwa kutuma au kupokea pesa kupitia tawi lolote la benki hiyo.

“Pindi unapotuma au kupokea pesa kuna kuponi utapewa na wafanyakazi wa benki katika tawi husika, unaijaza na moja kwa moja kuponi yako inaingia kwenye droo ya shindano hilo,” alisema.

Akishukuru kwa ushindi na zawadi hiyo, Ngulika alisema kompyuta hiyo itarahisisha shughuli zake za mawasiliano ambazo awali alikuwa akizifanya kupitia migahawa ya intaneti, mjini Iringa.

“Nilikuwa nalazimika kusafiri kutoka kijijini kwangu Tanangozi na kuja Iringa mjini kwa ajili ya kupata huduma hiyo. Sasa mawasiliano yangu na marafiki na ndugu zangu wa ndani na nje ya nchi, nitayafanya nikiwa kijijini kwangu,” alisema mzee huyo aliyewahi kufanya kazi na mashirika ya wakimbizi nchini.


Alisema amekuwa akifurahia kutumia huduma ya Western Union kupokea na kutuma fedha ndani na nje ya nchi kwa kuwa huduma hiyo ni ya haraka.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment