Tuesday, 14 November 2017

MKE AMSAFISHA MGOMBEA UDIWANI WA CHADEMA KATA YA KITWIRUMKE wa mgombea udiwani katika kata ya Kitwiru, Mjini Iringa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bahati Chengula, Veria Mwalo amepanda jukwaani kumsafisha mumewe dhidi ya propaganda alizoziita chafu zinazofanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kiaminike kwa wananchi.

“Wanasema nakuja kwenye kampeni za mume wangu baada ya kupewa pesa, wanaongopa mchana kweupe, kwanini nilipwe pesa na mume wangu ili nije kwenye kampeni zake, lakini wanashangaa kwanini situmii gari la mume wangu kwenye kampeni hizo, najiuliza nikitumia gari hilo linalotumiwa na mume wangu kwenye kampeni hizo, nitakutana saa ngapi na akina mama wenzangu wanaotusaidia kwenye kampeni hizi?” aliuliza na kusisitiza kwamba hiyo ni dalili ya kukosa hoja.

Alisema CCM pia imekuwa ikizusha kwamba mumewe ambaye ni mfanyabiashara anayejimudu yupo katika hatari ya kufirisika kwasababu ya madeni.

“Sijui taarifa hizi wanazipata wapi, benki au wapi? nachofahamu ni kwamba hakuna mali yoyote ambayo sisi tumeiweka kama dhamana mahali popote pale ili tupate mikopo, sasa hiyo hiyo taarifa wanaitoa wapi,” alisema.

Alisema mume wake ni mpambanaji, mwenye malengo aliyekuja Iringa Mjini kutafuta maisha na akayapata kwasababu ya juhudi zake anazotaka kuzitumia kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya kata ya Kitwiru.

“Kwasababu ya mtazamo wake wa hali ya juu katika maendeleo na kwa kuwa ni mtu asiyependa kushindwa ndio maana kagombea udiwani. Ana malengo makubwa katika kata hii, mchagueni ili mshirikiane naye kusukuma gurudumu la maendeleo, huyu hataki udiwani ili awe anapita kwenye majengo ya wafanyabiashara kuomba fedha za kujaza tumbo lake, hela za kujaza tumbo lake anazo,” alisema.

Alisema mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM Baraka Kimata ni mtu mwenye njaa, kigeugeu wa kisiasa anayetaka kuwatumia wananchi wa Kitwiru kujaza tumbo lake.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe alisema katika mkutano huo uliofanyika mtaa wa Uyole B jana kwamba; “Kitendo cha CCM kumsimamisha mgombea huyo, kimewafedhehesha wana CCM wa kata ya Kitwiru kwakuwa demokrasia ya kumpata waliyemtaka ilipindishwa.”

“Kimata sio chaguo la wana CCM wa kata ya Kitwiru, ni chaguo la viongozi walioamua kumlipa fadhila hiyo baada ya kukimbia Chadema na kujiunga na chama chao,” alisema

Reactions:

0 comments:

Post a Comment