Tuesday, 21 November 2017

MFAHAMU DC ASIA ABDALLAH NA ALIYOFANYA KILOLO MWAKA MMOJA NA NUSUJuni 2016, Rais Dk John Pombe Magufuli alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya mbalimbali nchini na mmoja kati yao alikuwa ni Afisa Tehama wa Wizara ya Fedha na Mipango, Asia Abdallah aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.Taarifa za uteuzi huo alizipata kupitia kwa marafiki zake wawili, Mark Tenda na Emmy Mbutu waliozisoma kupitia tangazo lililokuwa limetolewa na Ofisi ya Rais.

“Baadaye nilipigiwa simu ya kunitaka nifike ofisi ya Rais kwa ajili ya taratibu zingine ikiwepo kula kiapo cha uadilifu kama kiongozi,” anasema.

Mwaka mmoja na miezi minne imepita baada ya Julai 5, 2016 mkuu wa wilaya huyo kula kiapo hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza na hatimaye kuanza rasmi kuwatumikia wananchi wa Kilolo.

Katika salamu zake kwa wananchi wa Kilolo, Abdallah aliahidi kuzishughulikia changamoto mbalimbali za maendeleo ya wilaya hiyo kwa misingi ya haki na kwa kuzingatia sheria na maagizo ya viongozi wake wakuu.

Abdallah aliyefika mkoani hapa akiwa hana umaarufu, amekuwa maarufu kila kona ya mkoa wa Iringa katika kipindi kifupi cha uongozi wake yote hiyo ikitokana juhudi zake kubwa katika kushughulikia na kusukuma gurudumu la maendeleo ya wilaya hiyo na mkoa wa Iringa kwa ujumla wake, kwa mujibu ya watu wanaofuatilia utendaji wake kwa karibu.

Ndani ya kipindi chake na miaka miwili ya serikali ya awamu ya tano ya Dk John Magufuli, Abdallah anasema kasi ya maendeleo ni kubwa na hali ya wananchi kushiriki shughuli mbalimbali zinazowaongezea kipato inaongezeka.

Elimu
Anasema aliikuta wilaya ya Kilolo ikiwa katika hali isiyoridhisha kitaaluma na alichofanya kukabiliana na hali hiyo ni kuwapa hamasa walimu, wazazi na walezi kubadili mazingira hayo.


“Nilikuta baadhi ya shule zinawalalamikia wazazi na walezi wasiotaka watoto wao hasa wa kike wafanye vizuri kitaaluma kwa kuwa kuna tabia ya kuwaozesha wakiwa na umri mdogo na huwatumia kupata fedha pale watu wanapowataka kwa kazi za majumbani nje ya wilaya hii,” anasema.

Anasema baada ya kutangaza kuwachukulia hatua wazazi na walezi wenye tabia hizo, mambo yameanza kubadilika, kiwango cha elimu kinakua na ufaulu umeanza kuongezeka.

Akitoa mfano anasema ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 71.14 mwaka 2015 hadi asilimia 87.52 mwaka 2016, kidato cha sita asilimia 90 hadi 100, kidato cha pili asilimia 94.4 hadi asilimia 96.1 na darasa la saba asilimia 56 hadi asilimia 71.

“Lakini pia nimeshughulikia na kusimamia zoezi la kitaifa la utengenezaji wa madawati lililoasisiwa na Rais Dk Magufuli, na sasa tunaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya shule, madarasa, nyumba za walimu, maabara na kuainisha viwanja vya michezo,” anasema Abdalla ambaye pia ni shabiki wa mpira wa miguu akiishabikia Lipuli FC ya mjini Iringa.

Afya
Katika sekta ya afya, Abdalla anasema; “Mimi na timu yangu ya halmashauri ya wilaya tulianzisha upya mkakati wa kuendeleza ujenzi wa hospitali ya wilaya uliokuwa umesimama kwasababu ya ukosefu wa fedha ikiwa ni miaka miwili tu baada  ya kuanzishwa kwake mwaka 2011.”


Kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri hiyo, anasema Septemba, 2016 walifanikiwa kupata fedha toka serikali kuu zilizowawezesha kuendelea na awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali hiyo inayotarajiwa kuanza kutoa huduma zake wakati wowote mwakani.

Anasema awamu hiyo itakayotumia zaidi ya Sh Bilioni 4.2 hadi kukamilika kwake inahusisha ujenzi wa jengo la mionzi, jengo la kupokelea wagonjwa, jengo la utawala, jengo la huduma ya mama na mtoto, maabara na jengo la kulaza wagonjwa.


“Najua watu watauliza vipi kuhusu jengo la upasuaji na chumba cha kuhifadhi maiti. Niwajulishe tu kwamba tuko kwenye mipango hiyo, wakati wowote ujenzi wake utaanza kwa makubaliano ambayo tayari tumefanya na Suma JKT,” Abdallah anasema.

Anasema juhudi hizo hazijaishia kwenye ujenzi wa hospitali hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 230,000 wa wilaya hiyo lakini pia wanaendelea na maboresho ya vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya wilaya humo.

“Tangu nimeanza kazi wilayani Kilolo tumekamilisha ujenzi wa Zahanati mbili ya Kipaduka na Ndingisivile pamoja na wodi ya kulaza wagonjwa tuliyojenga kwa kushirikiana na kampuni ya New Forest,” anasema.

Kilimo
Kuhusu kilimo DC Abdallah anawahimiza wananchi kuachana na kilimo cha kujikimu na badala yake anawataka waingie kwenye kilimo cha biashara ili wajipatie kipato kikubwa zaidi kitakachobadili maisha yao na kuongeza tija kwa Taifa.


Anasema wilaya ya Kilolo ina ardhi nzuri na ya kutosha inayofaa kwa kilimo cha mazao ya biashara kama Chai, Kahawa, Pareto na mazao mengine ya chakula na mbogamboga kama mahindi, nyanya, vitunguu na matunda ya aina mbalimabli kama peazi na tufaha lakini pia inaanzisha kwa majaribio kilimo cha korosho katika kata ya Nyanzwa, Ruaha Mbuyuni na Mahenge.

“Serikali ya awamu ya tano inataka kujenga uchumi wa kati wa viwanda. Ujenzi wa viwanda unaendelea sehemu mbalimbali nchini na hata hapa kwetu Kilolo,” anasema.

 “Tunazo skimu za umwagiliaji tunazoendelea kuziboresha lakini pia tunajenga skimu nyingine ya Mgambalenga katika kijiji cha Mtandika. Kukamilika kwake kutawezesha zaidi ya hekta 2,000 kupata maji ya uhakika,” anasema.

Anasema Skimu hiyo itakayokuwa na urefu wa kilometa 17 inajengwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na zaidi ya Sh Bilioni 3 zinatarajia kutumika.

Lakini pia anasema katika kipindi chake cha uongozi wamepata ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) kwa ajili ya ujenzi wa skimu tano za umwagiliaji katika vijiji vya Nng’uruhe, Ihimbo, Lulanzi, Irindi na Kidabaga.

Ili sekta hii ifanikiwe, anasema mapambano yake ameyaelekeza kwenye uboreshaji wa miundombinu ya zamani na kuhakikisha mingine mingi mipya inajengwa.

Viwanda
Kuhusu viwanda, DC Abdallah anasema yeye na timu yake wamejikita katika kuhimiza wawekezaji wa ndani na wa nje kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo.

“Mbali na viwanda vidogo vidogo vingi, tayari tuna viwanda viwili vikubwa vimejengwa. Kimoja ni cha kuchakata mbao na magogo kinachomilikiwa na kampuni ya New Forest na kingine ni cha kusindika nyanya, kinachomilikiwa na kampuni ya Chai Bora maarufu kama Dabaga Vegetable,” anasema.


Abdallah anasema kiwanda cha cha Dabaga Vegetable kilichojengwa hivikaribuni katika kijiji cha Ikokoto kata ya Ilula, kimeanza uzalishaji huku kikinunua toka kwa wakulima kati ya tani 10 na 20 za nyanya kila siku kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na nyanya.

“Kujengwa kwa kiwanda hiki wilayani kwetu kunafungua fursa kubwa zaidi kwa wakulima wetu kuongeza uzalishaji wa nyanya na pilipili kwa kuwa soko linazidi kuongezeka,” anasema na kuongeza kwamba kiwanda hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Rais Dk John Magufuli wakati wowote kuanzia sasa.


Lakini pia wilaya ipo katika mkakati wa kujenga kiwanda chai ili kufufua kilimo cha zao hilo na anasema baadhi ya wadau likiwemo Shirika la Taifa la Hifadhi Jamii (NSSF) wameonesha nia ya kushirikiana nao.

Barabara
Anasema anasimamia kikamilifu ujenzi wa miundombinu ya barabara na kwamba kati ya mwaka jana na mwaka huu, barabara yenye urefu wa kilometa 3 imejengwa kwa kiwango cha lami wilayani humo.

“Nasimamia pia ujenzi wa barabara mbalimbali zinazojengwa kwa kiwango cha changarawe kwa kupitia fedha za serikali na kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) watakaosaidia kuboresha barabara zenye urefu wa kilometa 200. Ujenzi huo unakwenda sambamba na ule wa madaraja likiwemo daraja la kijiji cha Kiwalamo ambalo ujenzi wake ulisimama kwa zaidi ya miaka sita,” anasema.

Maji
“Nilipofika wilayani Kilolo moja ya kero kubwa niliyokutana nayo ni upatikanaji wa maji hasa katika mji wa kibiashara wa Ilula katika kata ya Ilula, tunaendelea na juhudi ya kumaliza changamoto hiyo,” anasema.

Anasema wakati mahitaji ya maji katika kata hiyo yenye wakazi zaidi ya 45,000 ni mita za ujazo 2,687; kwasasa maji yanayopatikana ni mita za ujazo 1,142 tu.

Anasema mwaka 2016/2017 serikali ilitoa Sh Milioni 800 kati ya Sh Bilioni 14 zinazohitajika kuwezesha kuanza utekelezaji wa mpango wa kuboresha huduma ya maji katika mji huo kwa kutumia vyanzo vya maji vya Mgombezi, Madisi na Kihoroto.


“Pia upo mkakati kabambe wa Serekali wa kumaliza kero ya maji maeneo ya Ruaha Mbuyuni ambapo ndani kipindi hiki cha 2015/2020 kero hiyo itakuwa imefikiwa kwa zaidi ya asilimia50,” anasema. 

Utalii
Mbali na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Hifadhi ya Misitu ya Asili ya Uzungwa na hifadhi ya Mazingira Asilia Kilombero, Abdalla anasema wilaya hiyo ina vivutio vingi na anawakaribisha wadau mbalimbali wajitokeze kuwekeza katika sekta hiyo.


“Nawahamasisha wadau mbalimbali wajitokeze kujenga miundombinu ya utalii, hasa hoteli ili kuvutia watalii wengi zaidi,” anasema na kuongeza kwamba wilaya hiyo ina maeneo ya kutosha yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.

Anataja fursa zingine zilizopo katika wilaya hiyo kuwa ni ufugaji wa samaki na nyuki, ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo cha chai, pareto, mazao ya mbogamboga na matunda, na madini ya dhahabu yaliyogunduliwa katika kata ya Ibumu, tarafa ya Mazombe.

Washirika wa wilaya
Anasema wilaya hiyo inazidi kupata mafanikio kwa ushirikiano na wadau wao mbalimbali wa maendeleo.


Anawataja baadhi ya wadau hao kuwa ni pamoja na viongozi wake wakuu wa serikali, viongozi na watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, vyama na viongozi wa kisiasa, na taasisi mbalimbali za kimaendeleo kama USAID, Mawaki, New Forest, Makota Forest, Asas pamoja na wananchi wa wilaya hiyo.

“Nawashukuru sana wananchi wa wilaya yangu ya Kilolo kwani ndio wadau wangu wakuu, tumekuwa tukishirikiana kikamilifu katika shughuli hizi  za maendeleo, wito wangu tuendelee kuunga mkono serikali ya Rais Magufuli kwani imedhamiria kuwapigania watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa,” anasema.

Changamoto
Anasema kwenye mafanikio hapakosi changamoto na kuzitaja baadhi zinazomchukiza kuwa ni pamoja na watendaji wazembe, tatizo la miundombinu ya baadhi ya barabara, ukatili wa kijinsia na ubakaji, na huduma hafifu ya usafiri wa abiria. 

Miaka miwili ya Dk Magufuli
Kuhusu miaka miwili ya serikali ya awamu ya tano ya Dk Magufuli, Abdallah anasema; “Ni kama miujiza ya mwenyezi Mungu, nchi kupata kiongozi anayetambua na kupambana kwa nguvu zake zote kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya wote lakini pia kiongozi anayejali shida za watu anaowaongoza.”
Image result for MAGUFULI IKULU DODOMA

 Anasema Dk Magufuli amekuwa kiongozi wa kuigwa na kila aliye chini yake anataka kufanya kazi kwa kutumia mbinu zake kwani zimedhihirisha jinsi zinavyorudisha maendeleo kwa Taifa na watu wake.

Anataja baadhi ya mambo yaliyofanywa na Dk Magufuli katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake kuwa ni pamoja na kurejesha nidhamu ya utumishi wa umma, vita dhidi ya rasilimali za nchi, ujenzi wa barabara za juu, bomba la mafuta, viwanja vya ndege, elimu bila malipo na mengine mengi.


“Nipongeze pia uamuzi wake wa kuhamishia makao makuu ya nchi kwenda Dodoma. Lilikuwa jambo lililoonekana kama haliwezekani, lakini limewezekana. Serikali sasa iko Dodoma,” anasema.

Maisha yake kwa ufupi
Asia Abdallah alizaliwa mkoani Dodoma  akiwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto wa nne wa familia ya Bwana na Bibi Abdallah.
Mbali na shahada ya TEHAMA, Abdallah mwenye mume na mtoto mmoja  ana shahada ya pili ya usimamizi wa biashara aliyoipata Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment