Monday, 20 November 2017

MCHUNGAJI MSIGWA ANOGESHA KAMPENI ZA UDIWANI KITWIRU


MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA) amesema chama chao kimemsimamisha mgombea makini, mwenye uwezo na mchapakazi hodari anayeweza kushirikiana vyema na wananchi wa kata ya Kitwiru kuleta maendeleo.

Katika uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu Chadema imemsimamisha Bahati Chengula dhidi ya mgombea wa CCM, Baraka Kimata anayetuhumiwa kwa usaliti baada ya kukihama chama hicho.

Msigwa anasema Baraka Kimata hakuwa mwanasiasa na ndio maana alihama kutoka Chadema akiwa na wadhifa wa udiwani na kukimbilia CCM ambako pia anatafuta nafasi ile ile.

“Huyu mtu tulimuokota Ipogolo akiwa  anashona nguo na alikuwa hajui chochote kuhusu siasa, tulimpika, akaanza kumudu jukwaa, akashinda udiwani, lakini kwa uroho wake wa fedha akahama Chadema. Anataka kuwatumia watu wa Kitwiru kujaza tumbo lake,” alisema Msigwa.

Msigwa aliwaomba wana Kitwiru kumchagua Bahati Chengula akisema atakuwa katika nafasi nzuri ya kushirikiana na baraza la halmashauri ya manispaa ya Iringa linaloundwa na madiwani wengi wa Chadema kuleta maendeleo ya kata hiyo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment