Tuesday, 14 November 2017

MAPOGOLO, MALIZANGA WATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA SPANEST


USHINDI wa Mapogolo FC katika yake ya kwanza ya Robo Fainali ya Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo wa 3-0 umetosha kuivunja timu hiyo hadi nusu fainali ya michuano hiyo, pamoja na kwamba jana ilipoteza mchezo wake wa marudiano kwa kupigwa bao 1-0.

Malizanga ilikuwa timu ya pili kufuzu hatua ya nusu fainali ya ligi hiyo jana, baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Idodi FC ambayo katika mechi ya awali ilipigwa bao 2-1.

Mechi za pili za hatua ya robo fainali zinaendeleo leo, Mboliboli FC ikiumana na  Itunundu FC na Kinyika FC wakipambana na  Ilolompya FC.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.


“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment