Wednesday, 15 November 2017

MALIZANGA YATINGA FAINALI KOMBE LA SPANEST, MAPOGOLO WATOTA
NDOTO ya Emmanuel Sade na timu yake ya Mapogolo FC kucheza fainali ya Kombe la Spanest Piga Vita Ujangili Okoa Tembo zimeyeyuka kama mafuta juu ya moto baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Malizanga FC.

Sade anakumbukwa katika mashindano hayo kwa kuwa mchezaji wa kwanza kupiga hat trick katika hatua ya robo fainali.

Malizanga ilishinda mchezo huo kwa kupitia mshambuliaji wake Panga Omary aliyeziona nyavu za Mapogolo katika Dk 23 na 42.

Goli la tatu la timu hiyo lilifungwa na David Mhanga katika Dk 74 huku Emanuel Sade akipachika bao la kufutia machozi katika Dk ya 54.

Kwa ushindi huo Malizanga analazimika kumsubiri mshindi kati ya Itunundu na timu kati ya Kinyika na Ilolompya itakayopatikana kwa maamuzi ya kamati ya mashindano hayo baada mchezo wa wa robo fainali kutofanyika kwa kile kilichotokana na mzozo wa wachezaji mamluki.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment