Thursday, 23 November 2017

LUKUVI AIKATISHA TAMAA CHADEMA AKIMNADI DIWANI WA KATA YA KIMALA
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), William Lukuvi ameongeza chachu ya ushindi kwa mgombea udiwani wa kata ya Kimala, wilayani Kilolo mkoani Iringa, Amoni Kikoti (CCM) katika kampeni za kumnadi mgombea huyo alizofanya jana.

Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi katika serikali ya awamu ya tano ya Dk John Magufuli anakuwa waziri wa pili kupambisha kampeni za uchaguzi huo mdogo wa udiwani utakaofanyika Jumapili, Novemba 26.

Alimnadi mgombea huyo anayepewa nafasi ya kushinda uchaguzi huo katika kitongoji kidogo cha Mhanga, Kilometa zaidi ya 100 kutoka Iringa Mjini na 42 kutoka Mgeta, Morogoro.

“Baada ya Mwigulu Nchemba kuja katika kata hii, Dk Magufuli kanituma na mimi nije nilete salamu kwenu, kwanza anasema anawasalimu sana na anawashukuru kwa kumpatia kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema.

Lakini pili, Lukuvi alisema Dk Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa anayo kazi kubwa na ngumu ya kuleta maendeleo ya Taifa na watu wake.

“Ili akamilishe kazi hiyo, anaomba aunganishiwe nguvu kwani katika baadhi ya maeneo daraja lake halijakamilika,” alisema.

Katika kukamilisha daraja hilo, Lukuvi alisema ni kwa wapiga kura wa kata hiyo kumchagua mgombea wa CCM katika uchaguzi huo mdogo wa udiwani.

“Mkimchagua Kikoti, mtakuwa mnaongea na mbunge wenu kupitia CCM Venance Mwamoto na Mwamoto ataongea na Rais kwa niaba yenu, na hatimaye kero zenu zitapatiwa ufumbuzi wa haraka” alisema.

Lukuvi alisema kwa kupitia Uchaguzi Mkuu wa 2015, Mungu aliipa baraka Tanzania kwa kuichagulia Rais anayeondoa machungu ya muda mrefu yaliyokuwa yakiwaliza watanzania.

“Tumepata Rais ambaye Mungu amemshusha atuondolee machungu ambayo hatukujua nani atayaondoa. Kama tungekuwa na Magufuli miaka 20 iliyopita huenda tungekuwa na lami hadi Kimala ambako ni zaidi ya Km 100 kutoka Iringa Mjini,” alisema.

Alisema baada ya Dk Magufuli kuchaguliwa watanzania wameanza kuona utajiri wa Tanzania, wanajua ukubwa wa rasilimali walizonazo na namna zinavyoweza kulineemasha Taifa kama zitasimamiwa inavyopaswa.

“Tanzania ina utajiri wa kila aina, ina ardhi kubwa, madini, wanyama, maziwa, mito, habari na rasilimali zingine nyingi ambazo kwa miaka mingi zimetumiwa na wajanja kujinufaisha na kunufaisha watu wengine,” alisema.

Alisema mfumo wa siasa chini ya utawala wa Dk Magufuli unazidi kubadilika kutoka kuhubiri uongo hadi ukweli.

“Miaka miwili ya magufuli imekuwa sawa na miaka 10 kwa wapinzani wa CCM kwani uongo waliokuwa wanauhubiri katika majukwa ya siasa sasa haukubaliki tena,” alisema.


Alisema siasa za umbea wa mjini, uongo, uzushi hazipo tena na hiyo inazidi kuwaweka wapinzani katika mazingira magumu ya kufanya siasa za ukweli na zenye hoja ya kujenga badala ya kubomoa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment