Saturday, 4 November 2017

LUGEGE AWAZAMISHA MABINGWA WATETEZI WA KOMBE LA SPANEST OKOA TEMBO
MSHAMBUALIJI Vais Ludege wa Tungamalenga FC anayefuatiliwa kwa ujirani na Lipuli FC ya Ligi Kuu Tanzania Bara, amewazamisha topeni mabingwa watetezi wa Kombe la Spanest Viga Vita Ujangili Okoa Tembo kwa kuwapachika bao mbili safi katika ushindi wao mnono wa mabao 4-0.

Mabao mengine ya Tungamalenga FC ambayo katika mechi yake ya awali na Kitisi FC walitoka sare ya 1-1, yalifungwa na Efrem Samila na Wile Mbwilo.

Msemaji wa Lipuli FC, Clement Sanga amesema timu yao imekuwa ikiyafuatilia mashindano hayo kwa karibu na tayari kuna baadhi ya wachezaji akiwemo Vais Ludege wanaweza kuchukuliwa kwa ajili ya kuimarisha timu ya vijana ya klabu hiyo.

Matokeo mengine ya jana Novemba 3 katika Ligi hiyo inayoshirikisha timu za vijiji 24 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, yaliyotolewa na Mratibu wa Spanest Godwell Ole Maing’ataki yalishuhudia Mapogolo FC ikimchapa kwa 1-0 Idodi FC kupitia kwa mshambuliaji wake Khalfani Kabonyera.

Katika michezo mingine iliyopigwa katika Tarafa ya Pawaga, Itunundu FC walimuazibu Kimande FC kwa bao 1-0 lililofungwa na Best Mambo katika Dk 28, nayo Isele FC iliibomoa ngome ya Kinyika FC katika Dk 28, kwa kuichapa bao 1-0 lililofungwa na Hamidu Mkosa.

Katika uwanja wa Mkombilenga, Mkombilenga FC ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Luganga FC, goli lililofungwa na Kefa Mkeza katika dk 21 ya mchezo.

Ligi hiyo inaendelea leo kwa Mboliboli FC kupimana ubavu na  Mbugani FC katika uwanja huru wa Kimande huku Nyamahana FC ikiwa mwenyeji katika uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Mafuruto FC.

Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na cheti, medali na Sh 500,000.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment