Saturday, 25 November 2017

LEO NDIO LEO FAINALI ZA KOMBE LA SPANESTMASHABAKI wa soka wanatarajia kujitokeza kwa wingi kushuhudia mtanange wa fainali ya Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili Okoa Tembo utakaopigwa katika dimba la Tungamalenga tarafa ya Idodi jioni ya leo.

Fainali hizo za nne za kombe hilo zinaikutanisha Malizanga FC ya tarafa ya Idodi na Itunundu FC ya tarafa ya Pawaga.

Malizanga wametinga fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mapogolo FC, mchezo uliopigwa Jumatano ya Novemba 15.

Itunundu wao wamefanikiwa kutinga fainali hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuwaondosha Kinyika FC kwa Bao 1-0 katika mchezo uliochezwa jana.

Pamoja na fainali hiyo, mashabiki hao watapata fursa pia ya kushuhudia mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na wanne utakaopigwa kabla ya fainali hizo kwa kuzikutanisha Kinyika FC na Mapogolo FC.

Mratibu wa SPANEST ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini Tanzania, Godwell Ole Meing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazmuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment