Tuesday, 21 November 2017

KINYIKA FC YAPETA KOMBE LA SPANEST, RUFAA YA ILOLOMPYA FC IKITUPWA


KAMATI ya mashindano ya Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili Okoa Tembo imetupilia mbali rufaa ya Ilolompya FC baada ya kujiridhisha kwamba haikuwasilishwa kwa kuzingatia kifungu cha rufaa namba 29.

Uamuzi huo ambao awali ulipingwa na Ilolompya, unaipa Kinyika FC Pointi 3 na mabao matatu ya chee na hivyo kuifanya icheze nusu fainali ya mashindano hayo dhidi ya Itunundu FC kesho.

Ilolompya na Kinyika walikuwa wakutane katika robo fainali ya kombe hilo, mchezo ambao hakuchezwa baada ya Ilolompya kutaka kutumia wachezaji mamluki.

Mshindi wa mchezo huo wa kesho atakutana katika fainali za michuano hiyo na Malizanga FC Novemba 25; mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Tungamalenga, Idodi.

Mgeni rasmi katika fainali hizo atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza atakayeongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa.

Mratibu wa SPANEST, amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment