Sunday, 26 November 2017

JK AWATUNUKU SHAHADA WAHITIMU CHUO KIKUU KISHIRIKI MKWAWA


RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete amepokewa kwa bashaha, nderemo na vifijo mjini Iringa juzi alipokuwa akiongoza mahafali ya tisa ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE).

Dk Kikwete aliyeingia katika viwanja vya chuo hicho kwa maandamano maalumu ya wanataaluma, alishangiliwa na wanafunzi na wageni mbalimbali wakati akielekea katika jukwaa kuu.

Katika mahafali hayo, Dk Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwatunuku wahitimu 1,101 waliofuzu shahada  mbalimbali ikiwemo ya elimu ya jamii na ualimu, sayansi na ualimu, elimu katika elimu ya jamii, elimu katika sayansi na stashahada ya uzamili katika elimu.

Mbali na kuwatunuku vyeti hivyo, Dk Kikwete hakuzungumza chochote na alaiki hiyo, hata pale wanahabari walipoomba kufanya naye mahojiano maalumu, walinzi na wasaidizi wake walikataa.

Awali Mkuu wa MUCE, Prof Bernadeta Killian alisema katika mahafali hayo kwamba chuo hicho kinakabiliwa na uhaba wa fedha za ufadhili kwa ajili ya kuwaendeleza wafanyakazi wake kitaaluma.

“Mathalani katika mwaka wa masomo wa 2017/2018 wafanyakazo 41 walichaguliwa kujiunga na vyuo katika ngazi mbalimbali za masomo lakini wameshindwa kutokana na ukosefu wa fedha za kugharamia masomo yao ambazo ni zaidi ya Sh Bilioni 1.4,” alisema akitoa taarifa hiyo kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kikwete.

Prof Killian alitaja tatizo lingine la chuo hicho akisema asilimia 70 ya wanafunzi wake wote wanaishi nje ya chuo kwasababu ya uchache wa mabweni,  hali inayowaweka wanafunzi hao katika mazingira kushindwa kufanya kazi zao kama wale wanaopata makazi ndani ya chuo.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya MUCE na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Rwekaza Mukandala alisema pamoja na changamoto hizo chuo hicho kimeendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa elimu ya viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Chuo pia kimefanikiwa kuanzisha program mpya mbili ambazo ni shahada ya umahiri ya sayansi na ualimu na shahada ya umahiri ya sayansi za jamii na ualimu,” alisema.

Alitoa pongezi kwa wahitimu hao kufuzu masomo yao vizuri akisema safari ya kusaka elimu si lelemama kwani inahitaji bidii, maarifa, kujituma na utiifu.

Katika risala yao iliyosomwa na Stoweka Sanga, wahitimu hao walikipongeza chuo hicho kwa mafanikio yake kitaaluma na waliishukuru serikali ya awamu ya tano ya Dk John Magufuli kwa kuonesha nia ya dhati ya kutatua changamoto hizo na zingine zinazoathiri kasi ya ufanisi wa malengo yake.

Sanga alizitaja changamoto zingine kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu, uhaba na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia masomo hasa ya sayansi na upungufu wa wahadhiri wa baadhi ya masomo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment