Friday, 10 November 2017

JENISTA MHAGAMA KUHUDHURIA KONGAMANO LA MAENDELEO GANGILONGA IRINGA


KATA ya Gangilonga, Iringa Mjini imemualika Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Kazi, Vijana Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kuhudhuria kongamano la maendeleo ya kata hiyo litakalojadili namna wadau wake watakavyoshiriki kushughulikia changamoto zake.

Mwenyekiti wa kongamano hilo, Askofu Owdenburg Mdegella alisema kongamano hilo litafanyika kesho Jumamosi katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU) cha mjini Iringa.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ubovu wa baadhi ya miundombinu yake ya barabara, uchafu, usalama, kazi, anuani za makazi na ajira.

“Tunapozungumzia maendeleo unagusa maisha ya watu. Ni mambo ambayo hayana dini wala itikadi yoyote ya kisiasa. Kwa hiyo tunataka watu wenyewe waseme ni kwa namna gani wanaweza kushughulikia changamoto zao,” alisema.

Pamoja na michango ya wananchi, wataangalia namna serikali na wahisani wengine kutoka ndani na nje ya nchi wanavyoweza kuchangia maendeleo ya kata yao.

“Katika kata hii ndiko anakoishi Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wengi wa serikali, ndiko iliko Ikulu ndogo lakini pia ni mahali wanakoishi watu wengi wanaoonekana kama waheshimiwa,” alisema.

Pamoja na uwepo wa waheshimiwa hao, Diwani wa kata hiyo, Dady Igogo (Chadema) alisema maendeleo ya kata hiyo hayalingani pia na uwingi wa taasisi mbalimbali zinazofanya shughuli mbalimbali mkoani Iringa.

“Katika kata hii kuna taasisi zaidi ya 300 zinazofanya kazi mbalimbali za maendeleo ya watu. Kwa kupitia kongamano hilo tutajadiliana namna pia zinavyoweza kushiriki kushughulikia changamoto zetu,” alisema.

Naye Mratibu wa kongamano hilo ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Fuad Mwasiposya alisema lengo lao ni kuona kata hiyo inafanana na kata zenye hadhi kubwa ndani na nje ya nchi.

“Tunataka iwe kata ya mfano nchini, kata itakayoingia kwenye ramani ya dunia ikiwa na watu wenye mwamko mkubwa wa kushughulikia changamoto zake,”


Reactions:

0 comments:

Post a Comment