Tuesday, 14 November 2017

ITUNUNDU YAINGIA NUSU FAINALI, ILOLOMPYA WAKISUSIA MECHI SPANEST CUP


ITUNUNDU FC imekuwa timu ya tatu kutinga nusu fainali ya Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo baada ya hii leo kuibamiza bila huruma Mboliboli FC kwa mabao 2-1

Mabao ya Itunundu yalifungwa na Ndumlila Mwenda katika dakika ya 2 na 33 ya mchezo huku Mboliboli ikipata goli la kufutia machozi katika Dk ya 23 kupitia kwa Jackson Mhumba.

Itunundu imefuzu hatua hiyo baada ya mechi ya kwanza na mahasimu wake hao kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Wakati huo huo mechi ya Kinyika FC na Ilolompya FC imeshindwa kuchezwa hii leo baada ya Ilolompya kukataa kucheza mechi hiyo bila wachezaji wake wanaodaiwa kuwa ni mamluki.

Kamati inayoratibu michuano hiyo itatoa uamuzi dhidi ya mzozo huo wakati mechi ya kwanza ya nusu fainali baina ya Malizanga na Mapogolo ikitarajiwa kupigwa kesho.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.

“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment