Sunday, 26 November 2017

ITUNUNDU FC YABEBA KOMBE LA SPANEST PIGA VITA UJANGILI, OKOA TEMBOITUNUNDU FC wametawazwa kuwa mabingwa wapya wa  Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo baada ya kuiadhibu Malizanga FC kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana kwenye uwanja wa Tungamalenga, Iringa Vijijini.

Kwa ubingwa huo, Itunundu wamepewa kombe, seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na watapata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Hadi mechi hiyo inakwenda mapumziko, Itunundu walikuwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa kwa penati na mshambuaji hatari wa Malizanga, Omari Panga katika dk 35 ya mchezo.

Katika kipindi cha pili cha mchezo huo uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, Itunundu walifanya mabadiliko ya mfumo kwa kujaza viungo wengi katikati na kuacha mshambuliaji mmoja mbele.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa timu hiyo iliyopata bao la kusawazisha katika Dk ya 67 kupitia kwa mshambuliaji wake Ndumulile Mwenda kabla Said Kisongozo hajaongeza bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya kufanyiwa faulo na walinzi wa Malizanga.

Mratibu wa SPANEST ambao ni mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania, Godwell Ole Maing’ataki alisema mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 24 tangu yazinduliwe Oktoba 21, mwaka huu yameshuhudiwa na mashabiki wa kandanda zaidi ya 200,000.

“Lengo la mashindano hayo yanayoshirikisha timu za vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni kuwahamasisha vijana kushiriki katika vita dhidi ya ujangili ili kuokoa Tembo na rasilimali zingine za hifadhi hiyo,” alisema.

Ushindi wa tatu wa mashindano hayo ulikwenda kwa Mapogolo FC walioinyuka Kinyika FC kwa mabao 2-0.

Malizanga ambao ni washindi wa pili, wameondoka na mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000 na mshindi wan ne akijinyakulia mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000.


Emanuel Sade wa Kinyika FC alijipatia Sh Sh 100,000 taslimu baada ya kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo akiwa na jumla ya magoli saba.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment